Nyong’o akiri viatu vya Raila ni vikubwa kwake katika ODM
KAIMU kiongozi wa chama cha ODM Anyang’ Nyong’o amekiri kwamba japo alikubali wadhifa huo, hawezi kufikia viwango vya mwanzilishi wa chama hicho, Raila Odinga.
Akizungumza alipowasili Kisumu Jumamosi baada ya uteuzi wake kuidhinishwa, gavana huyo aliwahakikishia wanachama kuwa kila kitu kitakuwa sawa, lakini akasisitiza haja ya umoja ili kukivumisha chama hicho.
“Nimeshukuru kuwa kiongozi wa chama changu Raila Odinga ambaye tumetembea naye kwa muda mrefu kuamua kunipa fursa na jukumu la kuongoza chama hiki wakati kama huu,” akasema Profesa Nyong’o.
“Mlisikia alichosema mwenyekiti Wanga(Gladys) kwamba uamuzi huu ulifanywa kwa kauli moja na chama chini ya mwongozo wa Bw Raila Amollo Odinga. Nilipofahamishwa uamuzi wa Kamati Kuu nilifikiri nilipewa mzigo ambao siwezi kuubeba ila kwangu kila kitu ninahesabu kama baraka.”
Kando na hayo, aliwarai wanachama kujiunga kwa manufaa ya wafuasi.
Lakini huku Gavana Nyong’o akichukua wajibu wa kukiongoza mojawapo ya vyama vikongwe na vilivyo na nguvu zaidi nchini, kiongozi huyo ana wajibu mkubwa kukabiliana na masuala mbalimbali katika chama hicho.
Kuanzia kutoridhika kwa maafisa wapya walioteuliwa kuongoza chama bila kiongozi wake, Bw Raila Odinga, misimamo tofauti kuhusu masuala na sera nyingi za kitaifa.
ODM ina ukuruba na serikali
Tangu Bw Odinga alipoamua kuungana na Rais William Ruto kurejesha utulivu nchini kufuatia misukosuko iliyosababishwa na maandamano ya Gen-Z Juni na Julai mwaka huu, Bw Musyoka ameendelea kuwaongoza vinara wengine wa Azimio kuukosoa utawala wa Rais William Ruto.
Kwa mfano, makamu huyo wa rais wa zamani amesimama kidete, kupinga mchakato wa kutimuliwa afisini kwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, mpango wa serikali wa ukodishaji wa Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA) kwa kampuni ya Adani na utekelezaji wa Bima mpya ya Afya ya Kijamii (SHIF).