HIVI PUNDE: Ruto ajibu kesi za Gachagua, ataka zitupiliwe mbali
RAIS William Ruto ameiomba Mahakama Kuu kutupilia mbali kesi kadhaa za kupinga kuondolewa kwa Rigathi Gachagua kama Naibu Rais, akidai kuwa masuala yaliyoibuliwa katika kesi hizo yametengewa Mahakama ya Juu pekee.
Dkt Ruto alisema katika majibu yake kwamba kesi zilizowasilishwa zinakiuka Kifungu 140 kama kinavyosomwa pamoja na vifungu vya 148 na 149 vya katiba, ambavyo vinatwika Mahakama ya Juu, mamlaka ya kuamua mizozo inayotokana na mchakato wa uchaguzi wa urais.
“Kwa mujibu wa Kifungu cha 165 (5) (a) cha Katiba, Mahakama hii haiwezi kuamua kesi na kutoa maagizo iliyoombwa, kwa kuwa ni suala ambalo limetengewa Mahakama ya Juu,” Dkt Ruto alisema kupitia wakili Adrian Kamotho.
Bw Gachagua na walalamishi wengine kadhaa walipinga mchakato wa kuondolewa kwake madarakani, kutokana na kutoshirikishwa ipasavyo kwa umma na kushindwa kuthibitishwa kwa madai yote dhidi yake.
Jaji Chacha Mwita na Richard Mwongo, wa Mahakama Kuu ya Milimani na Mahakama Kuu ya Kerugoya, mtawalia waliidhinisha kesi hizo kuwa za dharura na kusimamisha mchakato wa kujaza nafasi ya Bw Gachagua kama Naibu Rais.
Wiki jana, Mwanasheria Mkuu Dorcas Oduor na Bunge la Kitaifa waliwasilisha waliwasilisha kesi kupinga maagizo hayo na majaji Eric Ogola, Anthony Mrima na Freda Mugambi wakaagiza kesi hizo zitajwe Jumanne (leo).
Rais Ruto hata hivyo anataka kesi hizo zitupiliwe mbali akiteta kuwa zimewasilishwa kwa kupuuza sheria na ni matumizi mabaya ya utaratibu wa mahakama.
Bw Kamotho alisema kesi hizo zinakiuka Ibara ya 143 (2) ya katiba na mamlaka ya wazi ya Mahakama ya Juu kwamba rais hawezi kushtakiwa akiwa uongozini kuhusiana na jambo lolote analofanya au kutofanya chini ya katiba.
“Kesi iliyo hapa ina dosari isiyoweza kurekebishwa, inakiuka masharti ya sheria,” alisema.
Imetafsiriwa na BENSON MATHEKA