Amerika yashangaa hakuonekani kuwa na haraka ya kuunda IEBC
AMERIKA imelalamikia kucheleweshwa kwa mchakato wa uteuzi wa makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) wiki hii ambapo Mahakama ya Kuu ilibatilisha uamuzi wa Jopo la Kutatua Mizozo kati ya Vyama vya Kisiasa (PPDT) kuhusu suala hilo.
“Uwezo wa IEBC kuendeleza demokrasia nchini Kenya imo hatarini bila kuteuliwa kwa makamishna au bunge kutoa fedha za kufadhili usajili wa wa wapiga kura wapya, chaguzi ndogo na shughuli nyinginezo,” Balozi wa Amerika Meg Whitman alisema Jumatano.
Alisema hayo alipomtembelea Afisa Mkuu Mtendaji wa IEBC katika makao makuu ya tume hiyo Jumba la Anniversary, Nairobi, kujadili kuhusu “nyanja za ushirikiano” kati ya IEBC na Amerika.
Mnamo Jumanne, Mahakama Kuu ilibatilisha uamuzi wa jopo la PPDT uliomtangaza kiongozi wa Chama cha National Liberal Party (NLP) Dkt Augustus Kyalo kama mwakilishi wa vyama vilivyoko mrengo wa wachache bungeni katika jopo la kuteua makamishna wa IEBC.
Balozi Koki Muli na muungano wa Azimio la Umoja –One Kenya zilikuwa zimeelekea kortini kupinga uteuzi wa Bw Kyalo kuwa mwakilishi wa Azimio katika jopo hilo. Uteuzi huo wa kiongozi huyo wa NLP ulioungwa mkono na Kamati ya Kushirikisha Masuala ya Vyama vya Kisiasa (PPLC).
Baada ya Bi Muli na Azimio kukata rufaa, Jaji Janet Mulwa mnamo Jumanne Oktoba 22, 2024, alifutilia mbali uamuzi wa jopo la PPDT.
Katika uamuzi wake, Jaji Mulwa aliamuru kwamba uchaguzi mpya uendeshwe kuchagua mwakilishi wa Muungano wa Walio Wachache Bungeni, kulingana na Sehemu za 1 na 2 za Sheria ya IEBC, iliyofanyiwa marekebisho, ya 2024.
Aidha, Mahakama Kuu iliagiza kuwa uchaguzi huo ufanywe ndani ya saa 48 na sio baada ya saa tisa alasiri mnamo Alhamisi Oktoba 24, 2024.
Hii ni baada ya Mahakama hiyo kubaini kuwa Kyalo hakuteuliwa kwa njia halali kuwakilisha chama au muungano au chama cha walio wachache.
Ingawa uamuzi huo wa Mahakama Kuu ulionekana kurejesha ya shughuli ya kuundwa kwa jopo la uteuzi wa makamishna kukamilishwa, Dkt Kyalo alizamisha matumaini hayo kwa kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo.
Katika rufaa yake, kiongozi huyo wa chama cha NLP anataka utekelezaji wa uamuzi wa Mahakama Kuu usitishwe.
Aidha, Dkt Kyalo kupitia Katibu Mkuu wa chama hicho Omondo K’Oyoo Jumatano alimwandikia barua kiongozi wa Azimio Raila Odinga, akitaka apewe nafasi ya kushiriki katika mchakato wa uteuzi wa makamishna wa IEBC.