Habari za Kitaifa

Miadi na mwanaume asiyemfahamu vyema ilivyomletea mwanachuo mauti

Na MERCY KOSKEI October 26th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MWANAFUNZI wa Chuo Kikuu cha Mt Kenya ambaye mwili wake ulipatikana katika shamba la mahindi huko Kiamunyi, Kaunti ya Nakuru, alikuwa amesafiri kukutana na mwanamume waliyefahamiana kwa chini ya wiki mbili, Taifa Leo inaweza kufichua.Maut

Vivian Kajaya, mwanafunzi wa mwaka wa tatu, aliripotiwa kutoweka Oktoba 14 na marafiki zake na baadaye mwili wake kupatikana na wenyeji ambao walifahamisha polisi.

Rafiki yake ambaye aliomba tusimtaje jina alikumbuka kuwa Kajaya alidokeza kusafiri hadi Nakuru Oktoba 12 kukutana na mwanamume lakini akakataa kutaja jina lake.

‘Nilijaribu kumshawishi asiende kwani walikuwa hawafahamiani sana, lakini alikataa. Nilikuwa na wasiwasi kwa vile hakuwa na jamaa yeyote Nakuru lakini aliniambia lazima angeenda,’”rafiki huyo alisema akisimulia jinsi Kajaya alikuwa akijiandaa kwa safari walipozungumza mara ya mwisho.

Mwanamke huyo alipendekeza Kajaya aahirishe safari na hata akapendekeza waende pamoja lakini Kajaya alikataa akisema tayari alikuwa ameamua kwenda.

Saa sita mchana mnamo Oktoba 12, Kajaya, akiwa amevalia gauni la kijani kibichi na kubeba begi lake alilopenda zaidi la waridi, aliondoka kuelekea mjini Thika kutoka bweni laili kupanda matatu kuelekea Nakuru.

Baadaye, alimtumia rafiki huyo ujumbe saa tisa akithibitisha kuwa alifika salama. Kajaya alimwambia rafiki yake angemjulisha zaidi, na hata akajitolea kumweleza alilokuwa. Huo ndio ulikuwa mwisho wao kuzungumza.

Mwanamke huyo aliambia Taifa Leo kwamba alidhani kuwa kila kitu kilikuwa sawa hadi baadaye jioni hiyo hiyo wakati Kajaya alipompigia simu rafiki mwingine akisema bado alikuwa katika kituo cha basi cha Nakuru.

Alidai kwamba mwenyeji wake alikuwa amebadilisha mipango yao bila kutarajia.

Kajaya aliomba pesa za kurejea Nairobi lakini kabla ya marafiki zake kumsaidia, alipiga simu tena kusema kuwa mwanamume huyo alikuwa amefika na kumchukua mwendo wa saa kumi na moja na nusu jioni.

“Baada ya hakikisho hilo tulidhani yuko salama na tukalala. Lakini mwendo wa saa tisa usiku alimpigia simu rafiki yetu mwingine wa kiume na kumwomba asilale wala kuzima simu zake za rununu kwa kuwa alikuwa akirejea Nairobi akidai kuwa walizozana na mwanamume huyo,” rafiki huyo alisema.

“Tulikusanya vijana wengine ili tuweze kumchukua sote, tuliendelea kumsubiri lakini hakutupigia tena. Tulidhani labda alikuwa amebadilisha nia au wawili hao walikuwa wamerudiana na tukalala,” rafiki huyo alikumbuka.

Kufikia Jumapili, alikua na wasiwasi wakati simu ya Kajaya haikupatikana na jumbe hazikujibiwa.

Baada ya kujaribu kumtafuta Jumatatu, aliripoti kutoweka kwake katika Kituo cha Polisi cha Makongeni mjini Thika.

Muda mfupi baadaye aliona ripoti mtandaoni kuhusu mwili wa mwanamke uliopatikana Kiamunyi, Nakuru—mahali pale ambapo Kajaya alikuwa ametaja.

“Niliona begi aliloondoka nalo na hakika nilijua ni yeye. Baadaye ilithibitishwa, ‘alisema.

Wiki moja kabla, mwanamke huyo alisimulia kwamba Kajaya alkuwa amegombana na mwanamume huyo asiyeeleweka baada ya kukataa kumtumia nauli akishuku kuwa hangesafiri.

Hatimaye, walipatana na kupanga tena mkutano huo Oktoba 12. Siku chache kabla ya safari ya Nakuru, Kajaya alikuwa amekutana na mwanamume huyo huko Thika ambapo walitembelea hospitali moja na kufanyiwa vipimo vya Ukimwi.

Aliporudi, alimletea mwanamke huyo nguo mpya, mboga, na pesa taslimu.

Na kwa kutaka kujua kuhusu alikopata pesa hizo ghafla, rafiki huyo alimuuliza Kajaya na akamweleza kuwa alipatiwa na mwanaume huyo ambaye alimtaja kuwa tajiri na anayeendesha gari la Range Rover.

Siku iliyofuata, alimpigia tena simu wakakutana Juja, ambapo alimpa simu mpya yenye thamani ya Sh11,500.