Wanabiashara walilia serikali ya Nyeri iondoe marundo ya taka mjini
HUDUMA za kuzoa taka zimesitishwa katika miji mbalimbali kaunti ya Nyeri kwa muda wa wiki moja iliyopita huku serikali ya kaunti hiyo ikikosa pesa za kununua malori kwa huduma hiyo muhimu.
Wakazi wa miji ya Nyeri, Karatina, Othaya, na Naromoru miongoni mwa mingine wamelalamika kuwa taka hazijazolewa kwa muda wa wiki moja iliyopita.
Kaimu waziri wa huduma za afya katika kaunti hiyo James Wachihi hakujibu maswali yetu kuhusu hali hiyo.
Hakupokea simu wala kujibu ujumbe mfupi wa simu tuliomuuliza ni nini hasa kimesababisha kusitishwa kwa huduma hiyo.
Hata hivyo, duru katika idara ya utumishi wa umma ambayo mojawapo wa majukumu ni ukusanyaji wa taka zilisema kuwa serikali ya kaunti imekosa pesa na wizara ya fedha bado haijatoa pesa.
Wamiliki wa maduka katika Mji wa Karatina walilalamikia rundo la takataka ambazo hazijazolewa mbele ya maduka yao tangu wiki iliyopita.
Bw John Mwangi alisema hii si mara ya kwanza kwa uchafu kutupwa humo na kuziba lango la duka lake.
‘Kila wakati taka zikikosa kuzolewa wakazi hutumia sehemu ya mbele ya duka langu kama jaa ambapo kila aina ya taka hurundikwa,’ alilalamika.
Alisema mbali na kuwafukuza wateja kwa sababu ya uvundo, uchafu huo unahatarisha afya zao.