Wawili washtaki hoteli ya Travellers Beach wakidai walibaguliwa kwa misingi ya ngozi
KAMPUNI ya Dhanjal Investments Ltd inayomiliki hoteli ya Travellers beach huko Mombasa imeshtakiwa kwa madai kwamba maafisa wake wa ulinzi walibagua watu wawili- mwanamume na mwanamke.
Bw James Karugia na Grace Malila ambao wameshtaki hoteli hiyo wakitaka iamuliwe kwamba ilikiuka haki zao za kikatiba kwa kuwabagua.
Katika kesi waliyowasilisha katika Mahakama Kuu ya Mombasa, walalamishi hao wawili pia wanataka walipwe fidia ya jumla kwa mateso ya kiakili, dhiki, unyanyasaji na uvunjaji wa haki za kikatiba.
Wanadai kuwa mnamo Septemba 1 walitaka kuingia katika hoteli hiyo kupata chakula na shughuli zingine za burudani.
Wanasema katika lango la hoteli hiyo walisimamishwa bila sababu na kutakiwa kujitambulisha huku watu wengine waliokuja mbele yao wakiruhusiwa kuingia ndani bila kuchunguzwa wala kutakiwa kujitambulisha.
“Walalamishi hao walinyanyaswa na maafisa wa usalama mlangoni na kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji bila sababu na baada ya hapo walikatazwa kuingia hotelini,” wanasema katika kesi yao.
Wanadai kuwa watu wengine walioruhusiwa kuingia ndani ya hoteli bila kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji au mahitaji makali walikuwa watu wa asili ya Kieshia, Amerika au Ulaya.
Wanasema kuwa tabia ya maafisa wa usalama katika hoteli hiyo haikustahili, iliwadhalilisha na ilikuwa ubaguzi wa moja kwa moja dhidi yao kwa kuzingatia rangi ya ngozi zao.
“Walalamishi walifanyiwa dhihaka, fedheha na dharau kwa misingi ya rangi ya ngozi zao,” wanasema katika kesi yao.
Katika hati yake ya kiapo ya kuunga mkono kesi hiyo, Bw Karugia anasema kwamba anaishi Nairobi na alikuwa amesafiri hadi Mombasa mnamo Agosti 24 kwa biashara ambayo ilipangwa kudumu kwa wiki moja.
Aliendelea kusema kuwa mnamo Septemba 1 akiwa na Bi Malila alienda hotelini kupata chakula na burudani.
“Katika lango la hoteli ya Travellers Beach, tulizuiliwa na maafisa wa usalama bila sababu yoyote na baadaye tukaombwa kuonyesha vitambulisho vyetu,” asema Bw Karugia.
Bw Karugia anasema wakati hayo yakifanyika, aliweza kuona watu wengi wakiruhusiwa kuingia ndani bila kutakiwa kujitambulisha na bila ya kuhojiwa, kunyanyaswa au kuchunguzwa walivyokuwa wakifanyiwa.