Kocha wa Gor Mahia ahofia maisha yake baada ya timu kububundwa na City Stars
KOCHA wa Gor Mahia Leonardo Neiva ana wasiwasi kuhusu maisha yake baada ya kushambuliwa mjini Machakos na watu waliodai kuwa mashabiki wa klabu hiyo.
Neiva alishambuliwa na watu hao walidai kukasirishwa baada ya timu hiyo kushindwa 2-1 City Stars katika mechi ya Ligi Kuu iliyochezewa Kenyatta Stadium, Machakos.
City Stars ilikuwa haijashinda mechi yeyote tangu msimu uanze na pia ilikuwa haijashinda Gor Mahia tangu 2014 katika mechi 15.
Mjini Machakos, Gor Mahia ilichukuwa uongozi dakika ya 23 kupitia kwa Levin Odhiambo kabla ya Robin Asenwa kusawazisha muda mfupi baadaye.
City Stars chini ya ukufunzi wa Nicholas Muyoti walipata bao la ushindi kupitia kwa Dennis Oalo.
Mashabiki waliomfokea Neiva walimlamu kocha huyo kutokana na jinsi timu ilivyocheza vibaya kiasi cha kutoelewana uwanjani.
Ilibidi walinzi wa Gor Mahia kumsaidia kocha huyo pamoja na wachezaji kuhepa kunyongwa na mashabiki hao waliokuwa na ghadhabu huku wakimfokea kocha huyo aliyechukuwa mikoba kutoka kwa Johnathan McKinstry mnamo Julai 1.
Mlinzi Edwin Buliba wa City Stars alionyeshwa kadi nyekundu katika mechi hiyo dakika ya 88 kwa kumchezea ngware wing’a Shariff Musa.
Kabla ya kuandikisha ushindi huo, City Stars ilikuwa imetoka sare mara mbili na kushindwa mara tatu, 1-1 dhidi ya Sofapaka, kuchapwa 1-0 na Mara Sugar, kichapo cha 2-1 dhidi ya AFC Leopards na 2-0 dhidi ya Kakamega Homeboyz.
Gor Mahi iliyoanza mechi zake kama imechelewa kutokana ratiba ya michuano ya CAF ilikuwa imecheza tatu na kuandikisha ushindi wa 4-0 dhidi ya Mathare United katika mechi ya ufunguzi, 3-0 dhidi ya Posta Rangers kabla ya kuagana 0-0 na KCB.