Habari Mseto

Wasiwasi wasichana 52 wa shule wakitungwa mimba Mpeketoni

Na KALUME KAZUNGU  October 31st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

IDADI ya wasichana wa umri mdogo wanaoshiriki tendo la ndoa kutungishwa mimba kwenye tarafa ya Mpeketoni, Kaunti ya Lamu ni ya kushtua.

Ripoti ya hivi punde kutoka kwa shirika la kutetea haki za binadamu la Muslims for Human Rights (MUHURI) kwa ushirikiano na idara ya Afya na Hospitali katika Kaunti ya Lamu inaashiria kwamba jumla ya wasichana wadogo 52 walipachikwa mimba kwenye tarafa hiyo ya Mpeketoni kati ya Januari na Oktoba mwaka huu.

Msichana mdogo zaidi aliyeripotiwa kutungwa mimba eneo hilo akiwa ni wa umri wa miaka 13 pekee ilhali wengine wakiwa kati ya miaka 14 hadi 17.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo mjini Mpeketoni Jumatano, Mshirikishi wa MUHURI, Kaunti ya Lamu, Bi Kauthar Famau Abubakar alisema idadi hiyo hiyo ya wasichana wadogo 52 kupewa ujauzito pia ilishunudiwa mwaka 2023.

Alisisitiza haja ya wazazi kuwa mstari wa mbele katika kufuatilia mienendo ya watoto wao, hasa wasichana, na kuhakikisha wanawalea wakiwa na maadili mema.

Pia aliisihi jamii kuungana na kukemea wanaonyemelea wasichana wa umri mdogo kingono na kuwaharibia maisha yao.

“MUHURI kupitia mradi Shirikishi wa Masuala ya Kidini, Jamii na Mipango (JISRA) imeungana na idara ya Afya na Hospitali Lamu kuandaa ripoti hii kuhusiana na wasichana wetu wanavyoathirika na mimba za mapema hapa Mpeketoni, Lamu Magharibi. Takwimu zinaonyesha kuwa jumla ya wasichana wadogo 52 walipachikwa mimba mwaka huu wa 2024 wa umri mkubwa alikuwa miaka 17 ilhali mdogo zaidi akiwa miaka 13 pekee. Lazima tukomeshe dhuluma hizo kwa wasichana wetu ili kuwawezesha kusonga mbele kielimu,” akasema Bi Abubakar.

Ripoti hiyo inajiri wakati ambapo idara ya usalama, Kaunti ya Lamu tayari imejitokeza kutoa onyo kali kwa wanaume wanaonyemelea wasichana wa shule, kushiriki nao ngono na hata kuwabebesha ujauzito msimu huu wa likizo ndefu.

Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Bw Wesley Koech, pia aliwaonya wazazi na jamii dhidi ya kuficha visa vya wasichana wao wanapopachikwa mimba na kuwaoza kisiri badala ya kuwahimiza kuzingatia masomo.