Yafichuka baadhi ya makarani wa KTDA ‘hunyonga’ kilo kupunja wakulima wa majanichai
KATIBU wa Wizara ya Kilimo Paul Rono ameamuru uchunguzi ufanywe kuhusu visa vya ulaghai dhidi ya wakulima kwa kuvuruga mizani za kupima majani chai katika vituo mbalimbali Kusini mwa Bonde la Ufa na wahusika kuadhibiwa.
Hii ni kufuatia madai kuwa makarani wa Shirika la Ustawishajia Majani Chai (KTDA) huvuruga mizani za kupimia majani chai mabichi na hivyo kunakili uzani wa chini kuliko ule halisi.
“Serikali haitavumilia ufisadi na vitendo vya kuvurugwa kwa mizani ya kidijitali na hivyo kuwaibia wakulima. Wakulima wa majani chai hufanya kazi kwa bidii mashambani mwao hadi wanapowasilisha zao lao viwandani. Kwa hivyo, wanafaa kuchuma faida na hawafai kupata hasara,” Dkt Rono akasema.
Katibu huyo wa wizara alisema hayo baada ya kushuhudia kisa ambapo karani mmoja, mshukiwa wa uovu huo, alitoroka wakati wa ziara yake katika kituo cha Chepinyonyei katika eneo bunge la Ainamoi, Kaunti ya Kericho.
Karani huyo wa KTDA alitoroka akihofia kukamatwa na maafisa wa usalama walioandamana na Dkt Rono kwani ni mmoja wa wale wanaoshukiwa kuvuruga mizani ya kupimia majani chai kwa nia ya kuwalaghai wakulima.
“Mtu kama huyo anatoroka kwa sababu anafahamu kwamba ametenda kosa. KTDA isaidiane na maafisa wa usalama katika kufanikisha uchunguzi kuhusu uovu kama huu na wahusika wote wakamatwe na washtakiwe kwa mujibu wa sheria,” akasema Dkt Rono.
Bi Betty Korir, mkulima wa majani chai kutoka eneo hilo la Ainamoi, alikiri kuwa amewahi kulaghaiwa na makarani hao kwa njia hiyo.
“Siku moja nilipima majani chai yangu na kupata uzani wake ukiwa kilo 127, na hivyo kutimiza hitaji la kiwanda cha KTDA cha Chepinyonyei. Lakini baada kupimwa na makarani wa kiwanda hicho, nilishangaa nilipoletewa risiti iliyoonyesha kuwa uzani wa zao langu ulikuwa kilo 124, punguzo la kilo tatu,” akasema mama huyo wa watoto watatu.
Ili kuzima wizi huo, KTDA imesema kuwa imeweka kifaa cha kuzuia kuvurugwa kwa mizani katika viwanda vyote 71 inavyovisimamia kote nchini.
“Kifaa hicho huwekwa kadi maalum ya GSM. Huwa na uwezo wa kugundua jaribio lolote la kuvurugwa kwa mizani. Hutuma ujumbe kwa mameneja wa kiwanda endapo jaribio lolote litafanywa kuvuruga mizani yoyote,” alisema Mkurugenzi Mkuu wa KTDA anayesimamia Huduma za Usimamizi, Bw Collins Bett.
Kulingana na afisa huyo, kifaa hicho kitawezesha hatua za haraka kuchukuliwa dhidi ya washukiwa, na kwa wakati. Lakini kabla ya KTDA kuchukua hatua hiyo makarani waliopevuka katika nyanja ya teknolojia bado wamekuwa wakivuruga mizani hiyo na kuendelea kuwaibia wakulima wa majani chai.
Mnamo 2020, KTDA ilianzisha mizani ya kidijitali kuchukuwa nafasi ya zile za kawaida, kufuatia malalamishi kutoka kwa wakulima. Hii ni kufuatia pendekezo la jopo kazi lililobuniwa mnamo 2007 kuchunguza chanzo cha sakata hiyo ya kuvurugwa kwa mizani ya kupimia majani chai mabichi kwa nia ya kuwaibia wakulima.
Imetafsiriwa na CHARLES WASONGA