Ni rasmi Manchester United wamepata ‘dawa’ ya matokeo duni – Ruben Amorim
KUFIKIA Novemba 11, 2024, Ruben Amorim ataanza kazi rasmi kuongoza Manchester United baada ya kocha Mholanzi Erik ten Hag kupigwa kalamu.
Manchester United imetangaza kuwa imemsajili kuwa kocha mkuu hadi Juni 2027.
Kupitia taarifa, United wamemtaja kuwa ‘kocha mchanga mwenye mchezo wa kufurahisha na anayetajwa kuwa bora katika kandanda ya bara Ulaya.’
Hakuna shaka kuwa wasimamizi wa United wameona kazi yake ya kufana huko Sporting Lisbon, Ureno.
Ndio maana waliamua kuwapokonya mabingwa hao wa Ligi Kuu ya Kandanda Ureno meneja wao mpendwa.
Amorim hakutaka timu nyingine isipokuwa ‘mashetani wekundu’ endapo angeondoka kule Lisbon.
Duru pia zinasema United nao walimtaka kocha huyu huyu kwa jinsi anavyoonekana mchanga na mwenye mafanikio.
Siku ile ten Hag alimwaga unga, ndio siku ambayo ujumbe wa Manchester United ulipanda ndege kuelekea mji mkuu wa Ureno, Lisbon, kumshawishi Amorim ajiunge nao.
Klabu hii ilijua kilichohitajika kunasa huduma za Amorim ikiwemo pesa na kipindi cha kutoa notisi ya kuondoka ili kumtenganisha na Sporting pamoja.
Klabu ya United iliongea na ile ya Sporting, kisha Amorim akaamua kuvaa viatu vya ten Hag Jumatatu usiku.
Kufikia Jumatano, mkataba uliwekwa mezani ambapo Amorim na United walielewana kufanya kazi pamoja.
Sporting hawakutaka kumuacha kocha wao upesi vile. Walitaka angalau asimamie mechi nne likiwemo pigano la Klabu Bingwa Ulaya dhidi ya Manchester City juma lijalo.
Kwa sasa, klabu hii inaongoza katika jedwali la Primeira Liga kwa rekodi ya asilimia 100 – bila kushindwa.
Mabingwa mara 20 wa Ligi Kuu ya Kandanda Uingereza walifaulu kunasa huduma za Amorim majuma matatu kabla ya kipindi chake cha notisi kukamilika.
Mara yake ya kwanza kuongoza kikosi cha United katika ligi itakuwa katika mechi ya ugenini dhidi ya Ipswich Town Novemba 24.
Ufikapo wakati huo, Kaimu Kocha Ruud Van Nistelrooy atakamilisha kipindi cha kushikilia wadhifa kwa kusimamia mechi nne.
Katika siku kumi zijazo, Ruud atakuwa meneja kwa maandalizi ya mechi zitakazosakatwa Old Trafford dhidi ya Chelsea, PAOK na Leicester City – mechi za Ligi Kuu na Europa.
Duru kutoka United zinaarifu kuwa usimamizi uliongea na Amorim pekee na kuwa ndiye aliyekuwa chaguo la kwanza.
Manchester United hawakuchelea kumfuata hadi wampate kwa sababu kocha huyu alivutia pia mabingwa wa Uingereza Manchester City na Liverpool.
Kabla ya kuondoka kwa Erik ten Hag, Thomas Tuchel alikuwa anawindwa kuingia Old Trafford.
Haukupita muda mrefu kabla ya Uingereza kumsajili kuwa meneja wa timu ya taifa England maarufu ‘The Three Lions.’
Inaaminika kuwa United imenyakua huduma za Amorim baada ya kumuona akiwezesha Sporting kushinda mataji mawili ya ligi ya Ureno.
Anaonekana kuwa mkufunzi ambaye ana sifa tofauti na wale wa awali Old Trafford na kuwa ataleta mtindo mpya wa mchezo kama mfumo anaoupenda wa 3-4-3.