Habari za Kitaifa

Mlivyonitimua chapchap, tumieni kasi hiyo kupitisha mswada wa kahawa, Gachagua aambia bunge

Na CHARLES WASONGA November 2nd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

ALIYEKUWA Naibu Rais Rigathi Gachagua amewataka wabunge kutumia ile kasi na ‘weledi’ waliotumia kumtimua afisini kupitisha Mswada wa Kahawa wa 2023 unaolenga kuimarisha sekta hiyo.

Akiongea Jumamosi Novemba 2, 2024 katika Kaunti ya Kirinyaga, Bw Gachagua pia aliwataka wabunge kutumia kasi hiyo kupitisha Mswada wa Vyama vya Ushirika wa 2023.

“Ninatoa wito kwa wabunge wetu, haswa wale wanaotoka eneo hili kunakokuzwa kahawa kwa wingi, kwamba ile ‘speed’ ya kunitoa afisini watumie kupitisha mswada wa kahawa hadi usiku kisha  asubuhi yake wampelekee rais atie saini iwe sheria. Inavunja kuwa mswada huo umekuwa bungeni kwa kipindi cha mwaka mmoja,” Bw Gachagua akasema.

“Vile vile, wabunge wetu wapitishe Mswada wa Vyama vya Ushirika haraka ili sekta hiyo iweze kunyooshwa ndiposa ifaidi watu wetu,” akaongeza.

Bw Gachagua alisema hayo katika Kanisa la Kianglikana (ACK) la Kiamwathi, eneo bunge la Gichugu, alipohudhuria ibada ya wafu ya Anna Wanjiru, nyanyake Diwani wa Wadi ya Baragwi David Mathenge.

Aidha, naibu huyo wa rais aliyepoteza nafasi ya kujinusuru katika mahakama kuu, aliwataka wabunge kuishiniza serikali itoa Sh5 bilioni zilizotengwa kulipa madeni ya wakulima wa kahawa.

“Tulitenga Sh7 bilioni za kulipa madeni ya kahawa, kufikia sasa ni Sh2 bilioni zimetolewa. Kwa hivyo, ninawahimiza wabunge kuiwekea presha serikali itoe Sh5 bilioni zilizosalia ili wakulima wa kahawa wawe huru,” Bw Gachagua.

Alisisitiza kuwa viongozi wapewe nafasi ya kuwatumikia wakulima.

“Kazi niliyopewa na Rais ya kusimamia mageuzi katika sekta ya kahawa niliifanya kikamilifu. Hii ndio maana Mswada wa Kahawa uko bungeni. Kwa hivyo, kila kiongozi afanye kazi yake kwa sababu kile wananchi wanataka ni huduma,” Bw Gachagua akasisitiza.

Mbunge huyo wa zamani wa Mathira alivuliwa rasmi wadhifa wa Naibu Rais Ijumaa Novemba 1, 2024 kufuatia kuapishwa kwa Profesa Kithure Kindiki ili aanze kutekeleza majukumu ya afisi hiyo.

Kuapishwa huko kulijiri baada ya jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu kuondoa agizo la Jaji Richard Mwongo wa Kerugoya lililositisha kwa muda kujazwa kwa afisi ya Naibu Rais.