Chuo Kikuu cha Moi kufunguliwa tena huku matatizo ya kifedha yakikithiri
MATATIZO ya kifedha yanayozonga Chuo Kikuu cha Moi yanaendelea kukithiri baada ya Seneti kufeli kutatua suala la madeni ya mishahara ya wafanyakazi ya zaidi ya Sh10 bilioni.
Chama cha wahadhiri (Uasu) na kile cha wafanyakazi wa vyuo (Kusu) vimepinga pendekezo la Seneti la kufungua taasisi hiyo tena Novemba 4.
Badala yake vinataka kutekelezwa kwa mpango wa malipo ya mishahara na makato mengine.
“Hatuna haja na pendekezo la kufungua chuo tena kwa sababu hatukuhusishwa katika mazungumzo ya uamuzi huo. Tunachojua sasa ni kuwa mgomo unaendelea hadi usimamizi wa chuo utekeleze matakwa ya kulipa mishahara na makato mengine kikamilifu,” alisema Katibu wa Uasu Nyabuta Ojuki.
Kauli hii ilikaririwa na chama cha Kusu ambacho kimepinga kucheleweshwa kwa mishahara na kutowasilishwa kwa makato ya mikopo ya benki, pensheni na malipo mengine.
“Kufukia sasa, hakujakuwa na mwafaka kuhusu ufunguzi wa chuo kabla ya kulipwa kwa mishahara na makato mengine,” akasema Bob Odhiambo Ng’ura ambaye ni Mwenyekiti wa Kusu tawi la Chuo Kikuu cha Moi.
Usimamizi wa chuo hicho umepinga madai yaliyosambaa mitandaoni ya kuwepo kwa mpango wa kuhamisha wanafunzi hadi vyuo vingine kwa sababu ya matatizo makubwa ya kifedha.
“Tunataka kuhakikishia jamii yetu, wakiwemo wanafunzi na wazazi, kuwa madai hayo ni ya uongo,” alisema Prof Isaac Kosgey katika taarifa.
Prof Kosgey alipuuza notisi iliyovuma katika mitandao ya kijamii na iliyoonyesha imetiwa saini na Naibu Makamu Chansela Isaac Njuguna Kimengi akisema ni feki.
Haya yanajiri huku kukiibuka kuwa Seneti bado haijatangaza tarehe ya kufunguliwa tena kwa chuo baada ya kuchelewa kwa Hazina ya Kitaifa kutoa fedha zinazonuiwa kukinga chuo hicho dhidi ya kuporomoka.
Awali chuo hicho kilikiri kuwa katika hali mbaya huku madeni yakizidi zaidi ya Sh5 bilioni licha ya kuanza vianzo vya kutega uchumi ili kupata fedha za kusimamia shughuli zake.
Vyama vya wafanyakazi vimetuhumu usimamizi wa chuo kwa ‘kudharau maslahi ya wafanyakazi’ baada ya kutoa notisi ya kuwalipa sehemu ya mishahara na madeni.
“Hatujalipwa mishahara kwa zaidi ya miezi mitatu na hatuwezi kufanya chochote hata chuo kikifunguliwa,” alifoka Bw Ojuki.
Baraza la Chuo lilikuwa limepanga kufungua chuo tena mnamo Novemba 4. Mnamo Jumapili, Idara ya Elimu ya Juu ilitangaza kuwa chuo hicho kitafunguliwa Novemba 7, 2024 huku mashauriano yakiendelea na washikadau husika.
“Idara ya Elimu ya Vyuo na Utafiti itakuwa katika Chuo Kikuu cha Moi Ijumaa, Novemba 8, 2024 kuwakaribisha tena wanafunzi chuoni,” alisema Katibu wa Wizara Dkt Beatrice Inyangala kupitia taarifa katika akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa X.
Makamu Chansela Prof Kosgey alitangaza kufungwa kwa chuo mwezi uliopita kufuatia hali ya suitafahamu miongoni mwa wanafunzi baada ya wafanyakazi kugoma.
Wizara ya fedha inatarajiwa kutoa Sh2.9 bilioni ili kuokoa taasisi hiyo ya elimu inayokumbwa na changamoto za kifedha.
Imetafsiriwa na Labaan Shabaan