Habari Mseto

Mshukiwa wa mauaji ya wanawake 3 Eastleigh azuiliwa wabunge wakitaka vifo vitajwe janga la kitaifa

Na MARY WANGARI, RICHARD MUNGUTI November 5th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MSHUKIWA mkuu katika mauaji ya wanawake watatu waliotekwa nyara kutoka mtaani Eastleigh Nairobi alifikishwa katika Mahakama ya Makadara Nairobi Jumatatu Novemba 4, 2024 na kuagizwa azuiliwe kwa siku 21 kuhojiwa.

Mahakama ilielezwa maiti za wahasiriwa hao zilikuwa zimekatwa katwa na hata mmoja alikatwa viganja vya mikono yake yote miwili.

Hakimu mwandamizi Mary Njagi aliamuru Hashim Dagane Muhumed azuiliwe katika kituo cha polisi cha Ruaraka.

Wakati huo huo, kundi la wabunge sasa linaitaka serikali kutangaza visa vya mauaji ya wanawake ambavyo vimeongezeka pakubwa katika miezi michache iliyopita, kuwa janga la kitaifa.

Wabunge hao wanaojumuisha John Kaguchia (Mukurweini) na Wanjiku Muhia (Kipipiri) wamesema wanawake na wasichana sasa wanaishi kwa kuhofia maisha yao kutokana na visa vya mauaji vilivyokiri nchini.

“Wanawake, wawe wameolewa au la, wanaishi kwa hofu. Huwezi hata ukamtuma binti yako popote kwa kuhofia usalama wake. Wanawake ni walipa ushuru na kina mama wa mataifa, hata tukifanya maendeleo, yatawafaidi kina nani ikiwa tunawaua wanawake wetu? Alihoji Bi Wanjiku.

Wabunge hao wameashiria kidole cha lawama vyombo vya usalama, hususan idara ya ujasusi (NIS) na Idara ya Kukabiliana na Uhalifu (DCI) kwa utepetevu na kukosa kuzuia mauaji ya wanawake na wasichana yaliyokithiri nchini.

“Makachero wa DCI na NIS hutangamana na wanajamii na huweza kuwagundua wahalifu mapema kabla ya maovu kutekelezwa. Wako wapi siku hizi, ni bajeti hakuna? Ama wako lakini hawafanyi kazi,” alihoji Bi Wanjiku.

“Tunakumbuka hata enzi za utawala wa hayati rais mstaafu Moi, tulikuwa tunasikia kuhusu NIS. Walikuwepo lakini haungewaona na walijua kinachoondelea katika jamii. Wasichana wanapokuwa katika chumba fulani na kuna wahalifu na hakuna anayejua chochote hadi mmoja wao anapouawa au kutekwa nara, basi kuna tatizo. Kuna mtu hafanyi kazi.”

“Mauaji ya wanawake nchini tayari ni janga. Suala hili lilipaswa kutangazwa kuwa janga la kitaifa kitambo sana,” alisema Bi Wanjiku.

“Wanawake waliouawa wamefika hadi 100. Hata mwanamke kuuawa inatosha kuwa janga.”

Katika kisa cha Eastleigh, Sajini Mohammed alisema Dagane anachunguzwa kwa mauaji ya kinyama ya  Dahabo Daud Said, Musyaba Abdi Mohamed na Amina Abdirashid Dahir.

Baada ya kuuawa kinyama kwa wanawake hao maiti zao zilitupwa maeneo ya Kyumbi (Machakos) na mitaa ya Bahati na Parklands Nairobi.

Afisa huyo wa uchunguzi wa jinai alieleza mahakama kwamba ushahidi wa muda uliopo sasa ni kwamba mshukiwa huyo ndiye alionekana akitoka kwenye makazi yao.

Alikuwa akiendesha gari muundo wa Nissan Note nambari ya usajili KDQ 718Y.

Uchunguzi umebaini mshukiwa huyo aliwapigia simu wanawake hao simu kabla ya kuondoka nao wakiwa wameabiri.

Hakimu alielezwa na Sajini Mohammed kwamba baada ya kuwaua wanawake hao Dagane alipeleka gari hilo na kuliacha katika egesho la kampuni ya mabas ya Ena Coach Express.

Sajini Mohammed aliomba muda zaidi kuwezesha polisi kukagua picha za video na CCTV sawia na kuandikisha taarifa kutoka kwa mashahidi.

Afisa huyo wa uchunguzi wa jinai alisema  Dahabo Daud Said alionekana mara ya mwisho akiwa hai akitoka katika makazi yake mtaani Eastleigh Section III mnamo Oktoba 21, 2024 saa mbili usiku.

Hatimaye maiti ya Dahabo ilikutwa eneo la Kyumbi Machakos.

Viganja vya mikono yake vilikuwa vimekatwa na kutupwa.

Musyaba alionekana akitoka katika makazi yake Eastleigh Oktoba 22, 2024 akiandamana na Amina Abdirash Dahir.

Wote wawili walipatikana wameuawa.

Mwili wa Musyaba ulipatikana kando ya ua la shule ya msingi ya Bahati.

Ukaguzi ulionyesha alibakwa kabla ya kuuawa.

Mwili wa Amina ulikuwa umetupwa kando ya barabara ya Mwambao eneo la Parklands kaunti ya Nairobi.

Hakimu Njagi alikubaliana na Sajini Mohammed kwamba polisi wanahitaji muda kukamilisha uchunguzi.