Habari Mseto

Familia ya mwanariadha aliyedungwa kisu akafariki yaridhika na kifungo cha washukiwa

Na TITUS OMINDE November 6th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

WANAUME wawili waliopatikana na hatia ya mauaji ya mwanariadha Benjamin Kiplagat wa mbio za mita 3,000 za kuruka maji na viunzi mnamo Desemba 2023, wamehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 35 jela.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Eldoret, Bw Reuben Nyakundi, aliamua kwamba ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka ulihusisha Peter Ushuru, 30, na mwenzake mhudumu wa pikipiki David Ekai, 25, na mauaji ya mwanariadha huyo, mzaliwa wa Kenya ambaye amekuwa akikimbilia nchi ya Uganda.

Akitoa hukumu hiyo, Jaji Nyakundi alibainisha kuwa washtakiwa walimuua mwanariadha huyo kimakusudi hivyo walistahili adhabu kali.

Jaji Nyakundi alisema washtakiwa hao hawakujutia hata kidogo baada ya tukio hilo badala yake walijitetea licha ya ushahidi mwingi uliotolewa mahakamani na upande wa mashtaka kupitia picha za CCTV.

Picha hizo zilionyesha jinsi washtakiwa walivyomdunga kisu kifuani bila huruma na kumjeruhi moyo kabla ya kufariki papo hapo.

“Matendo yenu yalikuwa ya kikatili kwa mtu ambaye  hakuwa na uwezo wa kujilinda, kinyume na mpango wa Mungu ambapo Mungu alikusudia mwanadamu aishi kwa muda usiopungua miaka 70. Mahakama hii imewahukumu kila mmoja wenu kutumikia kifungo cha miaka 35 jela,” aliamuru Jaji Nyakundi.

Baada ya hukumu hiyo, familia ya marehemu ilipongeza mahakama, “Tuna furaha haki imetendeka ingawa tuliomba mahakama ihukumu maisha washtakiwa. Kama familia tumeridhika kwani tumetendewa haki ndani ya muda mfupi,” alisema Vincent Chemweno, ndugu wa marehemu.

Akitoa hukumu hiyo Jaji Nyakundi aliambia familia kuwa hakuna kifungo chochote kitakachochukua nafasi ya maisha yaliyopotea.