KPLC yapiga mnada jengo la Kanu kujilipa bili ya stima ya Sh212 milioni
BAADA ya kesi iliyochukua zaidi ya miongo miwili, jumba la Kanu House lililoko katikati mwa jiji la Nakuru limepigwa mnada baada ya wamiliki wake kushidwa kulipa bili ya stima ya zaidi ya Sh221 milioni ambayo usimamizi wake unadaiwa na kampuni ya umeme, KPLC.
Kulingana na Madalali wa Solai Auctioneers, walioteuliwa na KPLC kupiga mnada mali hiyo, kufikia Jumatatu, walikuwa wamepata mnunuzi ambaye alikuwa tayari kulinunua jengo hilo, linalomilikiwa na chama cha KANU, kwa Sh70 milioni.
“Tulipata anayetaka kulinunua jengo hilo la orofa mbili kwa Sh70 milioni, kufikia Jumatatu jioni mnada ulipofungwa. Pesa hizo ni za kununua jengo na ardhi ambako limejengwa,” akasema Bw Daniel Muturi wa Solai Actioneer aliyeendesha mnada huo.
Hata hivyo, thamani kamili ya mali hiyo iliyo na vyumba vingi vya kibiashara ni karibu Sh150 milioni.
Kampuni ya KPLC iliwasilisha kesi mahakamani mnamo 2004 dhidi ya chama cha Kanu.
Maafisa wa Kanu ambao majina yao yaliorodheshwa kwenye stabadhi ya mahakama ni Julius Sunkuli (aliyekuwa naibu katibu mkuu), Yusuf Haji (aliyekuwa mweka hazina), Bonaya Godana (Katibu Mpanga Ratiba).
KPLC ilidai kuwa Kanu ilifeli kulipa bili ya umeme kwa kipindi cha miaka minane.
Kampuni hiyo ya kusambaza umeme nchini ilitaka Kanu iamriwe ilipe Sh212,816,986 pamoja na riba, kuanzia tarehe ya kuwasilishwa kwa kesi hiyo.
Uamuzi wa kwanza kuhusu kesi hiyo ulitolewa mnamo Agosti 7, 2009 na Jaji J.B. Havelock.
Jaji huyo aliipata Kanu na kosa na kuiamuru ilipe malimbikizi yote ya bili ya stima iliyokuwa ikidaiwa na KPLC.