Habari Mseto

Wachimbaji madini wapokea ujuzi ili kukabili mabroka tapeli

Na KNA November 7th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

CHUO Kikuu cha Taita Taveta kimepanga warsha ya mafunzo kwa wachimbamigodi wadogo kutoka Kaunti za Kakamega na Vihiga ili kuwajengea uwezo wa kunufaika na biashara hii.

Mafunzo haya yanajikita katika mikakati ya kiusalama, matumizi bora ya vifaa vya kiteknolojia, hali yao ya maisha, jinsi ya kufaidika kutoka kwa uchimbaji madini, na umuhimu wa kuhifadhi mazingira.

Naibu Makamu Chansela wa Masuala ya Elimu, Kiakademia, Mafunzo na Mipango ya Kijamii katika chuo hicho Prof Christine Onyango, amesema jumuiya kubwa ya wachimbaji madini Kenya ni ya viwango vya chini lakini wanakosa ujuzi na maarifa yanayohitajika.

“Wachimbamadini wengi wa kiwango cha chini na wakati mwingi wanapunjwa na madalali,” anaeleza.

“Kuna haja ya kuwafunza umuhimu wa madini hizi na thamani yake ili mabroka wasiwatumbukize katika umaskini.”

Mbali na mafunzo ya stadi bora za utafutaji madini, wajasiriamali hawa walipokea mafunzo muhimu ya kifedha na uwekezaji.

Kama anavyoeleza Profesa wa Kilimo na Uchumi wa Maliasili Maurice Juma Ogada, kuna haja kubwa ya wachimbamigodi kulinda mazingira wanapochuma riziki.

“Hata wanapotafuta mkate wao wa kila siku, ni muhimu kwa wajasiriamali hawa kujua hazi za kinadamu zinazofungamana na kazi hii,” alisema.

Wakizingatia manufaa ya mafunzo haya, jumuiya ya wanaosaka madini magharibi ya Kenya inatoa wito kwa Chuo Kikuu cha Taita Taveta kuanza ushirikiano na taasisi za elimu ili kuendelea kujenga uwezo wao.

Vile vile, wameomba serikali ya kitaifa kushikana mkono na zile za kaunti ili kuwapa vifaa hitajika katika sekta hii.

Imetafsiriwa na Labaan Shabaan