Uchanganuzi: Misheni ya Kenya nchini Haiti yaweza kusitishwa lakini haitakuwa rahisi kwa Trump
HUENDA maombi ya Wakenya waliopinga hatua ya kuwapeleka maofisa wa polisi wa Kenya kutumika nchini Haiti yakajibiwa upesi, hasa kwa kuwa utawala wa Amerika utabadilika Januari 20, 2025.
Kuna dalili kwamba shughuli ya kudumisha amani na usalama itasitishwa haraka kuliko ilivyotarajiwa, na hilo likitokea, maofisa hao watarejea Kenya mapema.
Hii ina maana kwamba kuna uwezekano kuwa maofisa wengine 600 wanaofunzwa kukabiliana na magenge kabla ya kupelekwa Haiti hawatatumwa huko.
Donald Trump, ambaye alishinda uchaguzi wa urais wa Amerika wiki jana, anaendelea kuunda serikali yake itakayoanza kufanya kazi mara tu atakapoapishwa, na dalili zinaonyesha kwamba hatajali kuhusu masaibu ya mataifa mengine kama anavyofanya Rais Joe Biden.
Sera ya Trump kimataifa
Sera ya Trump ya mahusiano ya kimataifa hata alipokuwa rais miaka minne iliyopita ilikuwa kwamba Amerika ijiepiushe na mizozo ya nje ya nchi, ishughulikie masuala ya ndani pekee, ihifadhi dola za walipa-ushuru.
Teuzi za kwanza kabisa alizofanya Trump baada ya kuchaguliwa hivi majuzi zinaonyesha kwamba analenga zaidi kudhibiti mipaka ya Amerika na kuwazuia watu wanaoingia humo kinyume cha sheria.
Wakati wa kampeni zake, kiongozi huyo alionyesha chuki ya wazi dhidi ya raia wa Haiti wanaoishi Amerika, ilhali baadhi yao ni wahamiaji halali. Aliwasingizia kula mbwa na paka wa Waamerika, madai ambayo yaliwakasirisha wengi.
Ikizingatiwa kwamba hajali matatizo yanayoendelea nje ya mipaka ya Amerika, pamoja na kwamba anawachukia Wahaiti, inatabirika kuwa atawazuia kuingia Amerika, na hatatumia dola zozote kudhibiti hali nchini mwao, wakitaka waangamizane!
Shughuli ya kudumisha amani na usalama nchini Haiti inatekelezwa na polisi wa Kenya wakishirikiana na wenzao wa Haiti, na inagharamiwa kwa pesa za Amerika, ambazo Trump ameapa hazitatumika kuingilia mizozo ya nje.
Maofisa hao hawawezi kuendelea kutumika bila malipo, na Kenya haina uwezo wa kugharamia shughuli hiyo, kwa hivyo kuna uwezekano mkubwa kwamba maofisa wetu watafunganya virago na kurejea nyumbani.
Hii ni hali ya kutia hofu kwa kuwa huu ndio wakati ambapo Haiti inahitaji msaada wa maofisa hao kuliko wakati mwingine wowote.
Magenge mawili makuu yaliyogawana na kuitawala nchi hiyo kiubabe yameongeza harakati zao, na yameapa kukabiliana na maofisa hao.
Na, kana kwamba kuonyesha kuwa hayaogopi yeyote, Jumanne iliyopita magenge hayo yalishambulia ndege mbili za abiria, ambazo zinamilikiwa na kampuni za Amerika, U.S. Airlines na JetBlue.
Kampuni hizo zimetangaza kusitisha safari za ndege kutoka Amerika kwenda Haiti kati ya sasa na mwisho wa mwaka huu, na kuna uwezekano kwamba zitaacha kwenda huko kabisa hadi kuwe na serikali imara.
Ni kama ndoto ya mchana
Hiyo ya kuwa na serikali imara inasikika kama ndoto ya mchana kwa sababu tayari kuna mgogoro wa ni nani anayepaswa kuiongoza serikali kati ya kaimu waziri mkuu aliyefutwa, Dkt Gary Conille, na aliyeteuliwa kuchukua nafasi yake, Bw Alix Didier Fils-Aime.
Dkt Conille anasema alifutwa kinyume cha sheria kwa sababu ni rais pekee anayepaswa kumfuta. Ikumbukwe kwamba Haiti haijawa na rais tangu mwaka 2021, wakati ambapo Rais Jovenel Moise alipouawa, hivyo mwisho wa msukosuko huo hautabiriki rahisi.
Trump akiingia madarakani hatakubali kamwe kuziweka ndege za Amerika wala raia wake katika hatari ya kuangamizwa na magenge hayo.
Taifa jirani la Somalia lilipoingia machafuko na likakaa bila serikali kwa takriban miongo mitatu, Amerika ilikatisha safari zote za ndege na shughuli nyinginezo muhimu, maofisa wake wakawa wanafuatilia hali ya huko wakiwa Nairobi.
Ijapokuwa inatarajiwa kwamba Trump atakatisha shughuli hiyo ya kudumisha usalama na amani nchini Haiti kwa sababu ni mradi wa mtangulizio wake, huenda akauweka kwenye mizani pamoja na masaibu ambayo hatua ya kuukatisha inaweza kuiletea Amerika.
Amerika itaathirika kwa kiasi kikubwa
Akitambua kwamba Amerika itaathirika kwa kiasi kikubwa, hasa akijua Wahaiti watafurika Amerika kwa fujo, basi atakuwa radhi kutumia dola za Amerika kudumisha hali ilivyo sasa, mradi tu polisi au wanajeshi wa Amerika hawatakwenda Haiti.
Atautaja msukosuko huo kuwa suala la uhamiaji, na Waamerika wanaomwamini wataunga mkono hatua yake ya kutumia pesa zao kuwaweka mbali wahamiaji hao ili wasije kula mbwa na paka wao! Inaudhi, au kuchekesha, kutegemea msimamo wako kumhusu Trump.
Hilo likitokea, maofisa wa Kenya wanaotumika huko watakuwa wameponea, waendelee kupata mishahara minono, huku nayo serikali ya Kenya ikipata mgao wake kwa kukubali kusaidia katika tatizo hilo. Au ulidhani Kenya ilikubali kujihusisha na mzozo huo kwa hisani tu?
Utathmini
Kwa utathmini, jamii ya kimtaifa inapaswa kutafuta suluhisho la kudumu ili Haiti isigeuke kitega-uchumi kingine cha kimataifa kama Somalia.
Maofisa hao wa Kenya wanapaswa kupewa jukumu la kuwakamata viongozi wa magenge hayo, washtakiwe na kufungwa gerezani nje ya nchi, uchaguzi uandaliwe, Wahaiti wajitawale, wageni warejee kwao.
Vinginevyo, kuendelea kuikalia nchi ya watu kutawaudhi wenyeji na kuwahamasisha kujiunga na magenge hayo ili waendelee kupambana na wageni hao.