Habari za Kitaifa

Waziri ashangaza wabunge kutetea vikali Adani: ‘Hii Adani haina ufisadi na inalipa ushuru’

Na SAMWEL OWINO, JACK DENTON November 15th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

WAZIRI wa Uchukuzi Davis Chirchir alishangaza wabunge kwa kutetea vikali kampuni ya Adani ambayo inamezea mate kandarasi za mabilioni ya pesa, huku utendakazi wake ukiendelea kuibua lawama kote duniani.

Bw Chirchir aliambia wabunge kwamba Adani, ambayo imewasilisha zabuni ya kuboresha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) kwa kima cha Sh230 bilioni, na hivi majuzi ilitia saini mkataba mwingine wa kawi wa Sh96 bilioni wa miaka 30 na Kenya, haijapigwa marufuku katika nchi yoyote ile na inalipa ushuru kikamilifu.

Waziri aliambia Bunge kwamba kulingana na uchunguzi uliofanywa na serikali ya Kenya, Adani haijajihusisha na vitendo vyovyote vya ufisadi na haijafilisika.

“Adani haijajihusisha na ufisadi hadi sasa, haijafilisika na inazingatia ulipaji wa kodi kote, haijakosea katika uwajibikaji wake kwa jamii na ajira na wakurugenzi wake hawajapatikana na hatia kwa kosa lolote linalohusiana na maadili ya kitaaluma katika kipindi cha miaka mitano kabla ya kuwasilisha pendekezo lao,” Bw Chirchir alisema akitetea uamuzi wa Kenya wa kuzingatia mkataba wa ushirikiano kati ya sekta ya umma na ya kibinafsi.

Hata hivyo, licha ya hakikisho la Waziri, shughuli za utawala wa Rais Ruto na Adani zimepingwa mahakamani, ambayo imesitisha utekelezaji wa kandarasi hizo zenye utata.

Mwezi uliopita, Mahakama Kuu ilisitisha mkataba kati ya Kampuni ya Kusambaza Umeme Kenya (KETRACO) na Adani Energy Solutions ya kujenga na kuendesha miundo msingi ya umeme inayojumuisha laini za kusambaza stima.

Mahakama Kuu iliagiza serikali kusitisha mkataba wa miaka 30 na kampuni ya Adani Energy Solutions hadi itakapoamua kesi iliyowasilishwa na Chama cha Wanasheria nchini Kenya kupinga mkataba wa ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi.

Mapema Septemba, Mahakama Kuu pia ilisimamisha kwa muda mipango iliyopendekezwa ya kukodisha JKIA kwa Adani kwa miaka 30.

Mnamo Jumatano, Bw Chirchir aliambia Bunge kwamba kwa kufuata kikamilifu maagizo ya mahakama ya kusitisha mpango huo, serikali haijaingia katika mkataba wowote wa makubaliano na Adani.

Aliwaambia wabunge habari zote kuhusu mpango huo zimetolewa kwa washikadau wote na Seneti. Bw Chirchir alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Gatanga, Bw Edward Muriu, aliyetaka kujua ikiwa serikali ina makubaliano yoyote na Kampuni ya Adani kuhusu JKIA.

Mbunge huyo pia alitoa changamoto kwa Waziri kuwasilisha ushahidi wa ushiriki wa umma, kueleza kama makubaliano hayo yalizingatia masharti ya kikatiba kuhusu utawala na ufichuzi kamili wa taarifa zote kuhusu mkataba huo wenye utata.

Bw Muriu alipinga madai ya waziri ya kutakasa kampuni zinazohusiana na Adani.

“Nimeshangazwa na taarifa kutoka kwa Waziri kwamba Adani haina kesi ya ufisadi na inalipa kodi kwa sababu kulingana na stakabadhi, Adani imezuiwa kufanya biashara nchini Australia, India kwa sababu hizo hizo tunazozungumza,” Bw Muriu alisema.

Mbunge huyo alitakiwa kuwasilisha ripoti hiyo lakini alipoiwasilisha, Spika Moses Wetangula alisema ukweli wake hauwezi kuthibitishwa.

“Nimeangalia stakabadhi na hazikubaliki. Ukitaka zizingatiwe, unajua la kufanya,” Bw Wetang’ula alisema.

Mbali na agizo la mahakama la kusitisha utekelezaji wa mkataba huo, Kamati ya Bunge ya Kitaifa ya Uwekezaji wa Umma inayoongozwa na Mbunge wa Pokot Kusini David Pkosing pia imetaka mpango huo uchunguzwe kwa kina.Kamati hiyo inamtaka Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Nancy Gathungu kuchunguza jinsi Adani alikabidhiwa mkataba huo na kuionya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini Kenya dhidi ya kutia saini mkataba huo kabla ya ripoti ya ukaguzi wa uchunguzi kuwasilishwa na kujadiliwa na Bunge.

Huku mzozo ukiendelea katika Bunge la Kenya, kampuni ya Adani imezua utata zaidi nchini Bangladesh ambapo imesababisha kukatwa kwa umeme katika taifa hilo jirani, likitaja malipo yaliyochelewa yanayokadiriwa na kundi hilo kuwa takriban dola 850 milioni.

Adani Power imekuwa ikisambaza umeme Bangladesh kutoka kwa mtambo wake wenye uwezo wa megawati 1,600 mashariki mwa India na ilikuwa imetishia kukata usambazaji wote ikiwa bili haingelipwa.

Mnamo Machi mwaka huu, Bloomberg News iliripoti kuwa Amerika ilikuwa imepanua uchunguzi kuhusu Adani kufuatia madai ya utoaji hongo.

Kulingana na ripoti hiyo, waendesha mashtaka walikuwa wakichunguza ikiwa shirika la Adani au watu wanaohusishwa na kampuni hiyo walihusika katika kuwahonga maafisa nchini India ipendelewe katika mradi wa nishati.

Lakini Adani Group iliiambia Bloomberg News: “Hatuna habari kuhusu uchunguzi wowote dhidi ya wakurugenzi wetu.”

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA