Habari za Kitaifa

Ruto aonya Maaskofu wa Kanisa la Katoliki

Na RUSHDIE OUDIA November 15th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

RAIS William Ruto amewakashifu viongozi wa makanisa kwa kuukosoa utawala wake akisema wanafaa kuwa waangalifu wasije wakaathiriwa na kile wanachosema.

Dkt Ruto alikuwa akijibu taarifa iliyotolewa siku ya Alhamisi, Novemba 14, 2024 na Maaskofu wa Kikatoliki walioitaka serikali ya Kenya Kwanza kuwajibika.

Maaskofu hao chini ya muungano wao wa KCCB, walilalamikia kuongezeka kwa mzigo wa ushuru, kupanda kwa gharama ya maisha, ufisadi, malalamishi kuhusu sekta ya afya, kuongezeka kwa ukiukaji wa haki za binadamu kufuatia utekaji nyara na mauaji kiholela.

Maaskofu wa Kikatoliki wanahisi kuwa badala ya serikali ya Kenya Kwanza kushughulikia malalamishi yaliyotolewa na Wakenya, imetumia uongo, kutoza ushuru wa juu na kushughulikia mambo ambayo hayawafaidi Wakenya.

Katika ujumbe wake ambao pia alielekezea Wakenya kwa jumla na viongozi wa kisiasa ambao wamekuwa wakimkosoa katika siku chache zilizopita, Rais Ruto alionekana kujitetea, akisema kuwa wanaomkosoa wanafaa kuzingatia ukweli na kufanya hivyo kwa tahadhari.

Akizungumza Ijumaa, Novemba 15, 2024 jijini Nairobi, Dkt Ruto aliwaomba makasisi na viongozi kujitahidi kuifanya Kenya kuwa nchi ambayo wote wanaweza kujivunia.

Aliwataka wanaoukosoa utawala wake kuwa na ushahidi.

“Ninataka kusihi kila mtu ikiwa ni pamoja na makasisi kwamba hata tunaposhiriki katika masuala ya mazungumzo ya umma na mambo muhimu sana kwa Wakenya, tunapaswa kuwa waangalifu ili kuwa wa kweli tusije tukaathiriwa na kile tunachokosoa,” Dkt Ruto alisema.

Matamshi ya Dkt Ruto yalijiri wakati ambapo anakabiliwa na ukosoaji mkubwa kutoka kila sehemu kwa kutotimiza ahadi zake za kampeni.

Kanisa, matabibu, viongozi wa upinzani, aliyekuwa Naibu wake Rigathi Gachagua, walimu, baraza la Magavana, wanaharakati wa haki na wanafunzi wa vyuo vikuu wote wamekuwa wakiibua wasiwasi mbalimbali ambao ni pamoja na kutolipwa mishahara, mgawanyo usio wa haki wa rasilimali, ufisadi na uzembe katika kuendesha shughuli za nchi.

Mara tu Maaskofu walipomaliza mkutano wao na waandishi wa habari, serikali ilijaribu kujitetea kwa kila pande.

Kulikuwa na taarifa ya Waziri wa Afya Deborah Barasa akisema serikali haikubaliani na kile alichotaja kama “taarifa za kupotosha na za uongo” za maaskofu wa Kanisa la Katoliki.

Mwenzake wa Elimu Bw Julius Ogamba pia alikanusha ripoti kwamba mfumo wa elimu nchini umedorora, akisema wamechukua kila hatua katika kutekeleza mapendekezo ya Rais kuhusu mageuzi ya elimu, na zaidi hasa kwa Shule za JSS na Mtaala wa CBC.

Mbunge wa Kapseret, ambaye ni mwandani wa karibu wa Dkt Ruto pia kupitia akaunti zake rasmi za mitandao ya kijamii alikashifu vikali taarifa ya Maaskofu wa Kikatoliki.

Imetafsiriwa na Winnie Onyando