Walimu wataka Kajiado itangazwe eneo la mazingira magumu ya kazi
CHAMA cha Kitaifa cha Walimu (KNUT) kimeomba Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) kurejesha utambuzi wa Kaunti ya Kajiado kama eneo lenye mazingira magumu ya utendakazi.
Hii itawawezesha walimu katika kaunti hiyo kulipwa marupurupu ya kuhudumu katika mazingira magumu sawa na wenzao wanaofanya kazi katika maeneo kame (ASAL).
Akiongea alipohudhuria mkutano wa kila mwaka wa Knut tawi la Kajiado, Katibu Mkuu wa chama hicho Collins Oyuu alisema walimu wanaofundisha Kajiado wanapitia changamoto nyingi kutokana na mazingira magumu wanayofanyia kazi.
“Kajiado ingali eneo lenye ugumu kwa wafanyakazi wakiwemo walimu. Lakini inasikitisha kuwa TSC iliondoa Kajiado kutoka orodha ya kaunti ambako mazingira ya utendakazi ni magumu,” akasema Bw Oyuu.
Katibu huyo Mkuu pia aliilaumu TSC kuwa kukosa kuwatuma walimu wa kutosha katika maeneo kame, akisema hiyo inaathiri viwango vya elimu.
Bw Oyuu aliitaka tume hiyo iajiri walimu zaidi kuwezesha kifikiwa kwa idadi hitajika ya walimu kwa mujibu wa viwango vilivyowekwa na Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Elimu na Utamaduni (UNESCO).
“Tunaitaka serikali iajiri walimu zaidi ili kupunguza kero ya uhaba wa walimu wa kutosha kote nchini. Inasikitisha kuwa katika baadhi ya shule mwalimu mmoja anawafunza watoto 70 badala ya wanafunzi 45, kulingana na viwango vya Unesco,” Bw Oyuu akasema.
Katibu wa Knut katika Kaunti ya Kajiado Elie Korinko alisema shule zilizoko maeneo ya mijini zina walimu wengi kupita kiasi ilhali zile zilizoko mashambani zinakumbwa na uhaba mkubwa wa walimu.
“TSC inafaa kudumisha usawa wakati wa usambazaji wa walimu. Shughuli hii haistahili kuyumbishwa kwa manufaa ya maeneo fulani pekee huku maeneo mengine yakiumia,” akasema.
“Kwa hivyo, tunaitaka TSC kuendesha shughuli ya kutumwa kwa walimu kwa njia inayozingatia usawa na uwazi,” akaongeza.
Mapema mwaka huu, TSC ilitekeleza mpango wa usawazishaji ili kutoa nafasi kwa makundi yaliyobaguliwa katika sekta ya elimu kupata haki.
Waliofaidi ni walimu kutoka makabila madogo yaliyotengewa, wanaoishi na ulemavu na walimu kutoka maeneo yaliyosalia nyuma kimaendeleo.
Aidha, kaunti nyingine zaidi zilijumuishwa kwenye orodha ya zile zenye mazingira magumu ya utendakazi.