MakalaMichezo

Amorim aanza kuwanoa wachezaji wa Manchester United

Na LABAAN SHABAAN November 19th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KOCHA Mkuu wa Manchester United Ruben Amorim ameanza kuwanoa wachezaji wa timu hiyo inayosakata kambumbu ya kulipwa nchini Uingereza.

Awamu ya kwanza ya mazoezi chini ya mkufunzi mpya wa asili ya Ureno ilianza Jumatatu kuhusisha wachezaji ambao hawakushiriki mashindano na timu zao za taifa.

Kipindi cha mapumziko ya michuano ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kinaendelea na makabiliano yatarejelewa tena wikendi hii.

Mechi ya kwanza atakayosimamia Amorim itagaragazwa Jumapili ijayo ugenini ugani Portman Road dhidi ya Ipswich Town.

Kinda matata Kobbie Mainoo anaendelea kurejesha hali yake bora alipoanza kufanya mazoezi na wachezaji wenzake.

Mainoo alikuwa anauguza jeraha baada ya kuumia Red Devils ilipokabana koo na Aston Villa mnamo Oktoba.

Amad Diallo vile vile alishiriki kipindi hiki cha mazoezi baada ya kukaa nje ya kikosi cha Ivory Coast kwa sababu ya jeraha aliyopata dhidi ya Leicester City.

Walinzi Luke Shaw, Tyrell Malacia na Lenny Yoro pia walikuwa katika awamu ya kupata makali huku wakiendelea kufikia utimamu wa kushiriki mechi za ligi.

Lisandro Martinez na Victor Lindelof wamerejea Carrington juma hili ili kutathminiwa baada ya kuaga vikosi vyao vya timu ya kitaifa za Argentina na Uswidi mtawalia.

Amorim hakuweza kupata timu kamili katika siku yake ya kwanza ya mazoezi kwa sababu wengine wanachezea timu zao za taifa kipindi cha mapumziko ya EPL.

Kwa hivyo, ilibidi apate ziada ya wachezaji wengine kutoka kwa akademia ya United ili kufanya mazoezi na wachezaji kumi wa timu ya kwanza waliokuwa uwanjani.

Kocha huyo wa hivi punde zaidi wa Sporting Lisbon atapata timu ya kwanza kamili baadaye juma hili watakapomaliza kusakatia timu zao za taifa.

Amorin anayeshabikiwa sana kwa kulea vipaji vya soka alihusisha kinda nyota Godwill Kukonki, 16, katika mazoezi hayo.

Kukonki amekuwa akifana katika msimu mpya wa timu ya chipukizi wa U18 na amepewa nafasi ya kupepeta boli na wachezaji wa timu ya kwanza kwa mara ya kwanza.

Kwa kawaida, mastaa wachanga huitwa kushiriki mazoezi na timu ya kwanza kunapohitaji wachezaji zaidi Carrington.

Difenda huyu mwenye kimo kinachohitajika kwa walinzi, anatarajiwa kumvutia Amorim.

Tayari Kukonki ameanza kufananishwa na mchezaji wa Manchester City Josko Gvardiol.

Anaonekana kuwa mchezaji adimu kupata kuzingatia anacheza kwa mguu wa kushoto katika safu ya katikati ya ulinzi.

Walinzi wanaotumia miguu ya kushoto wanathaminiwa sana katika kandanda ya sasa.

Ndiyo sababu Manchester United walijaribu kuwasilisha dau kunyaka huduma za difenda wa Everton Jarrad Branthwaite.