Bingwa wa ‘Mali Safi Chito’ atafuta ‘nyota yake’, alipua ngoma mpya ‘Sherehe Kikwetu’
MWIMBAJI anayetambuliwa kwa nyimbo maarufu ‘Mali Safi Chito’, Marakwet Daughter, ameachia kibao kipya akiamini kitamrudisha kuwa gumzo katika ulingo wa burudani.
“Wimbo huu ni bora katika misimu ya sherehe na utaburudisha watu sana wanapofurahia ufanisi wao,” Marakwet Daughter akasema katika mahojiano na Taifa Leo kwa njia ya simu.
“Mashabiki wamependa kibao hiki sana hasa kwa sababu ya kufaa sherehe,” aliongeza. “Ni ngoma ambayo imetulia na inachangamsha mashabiki.”
Tulipomchokoza kuhusu kufifia kwa mashabiki baada ya kuvuma kwa ‘Mali Safi Chito’, alisema: “Mimi sijapoteza nyota kwa sababu nimekuwa katika ulingo wa muziki kwa miaka 16. Watu ambao walinijua juzi ndio wanadhani nimezama kimuziki.”
Alizindua ngoma hiyo inayokwenda kwa jina ‘Sherehe Kikwetu’ Novemba 8, 2024 bila video na kupakia katika mtandao wa kupeperusha video wa YouTube.
Haikuchukua muda kabla ya Marakwet Daughter kufyatua video ya kibao hicho.
Alipakia video yake Novemba 13 na tayari imeanza kuvuna mashabiki lengwa wanaoitumia katika shamrashamra na kujifurahisha katika mitandao ya kijamii hasa TikTok.
Marakwet Daughter ameonekana kushuka bei kimuziki baada ya kuvuma kwa kibao ‘Mali Safi Chito’ Novemba 2023 na sehemu kubwa ya mwaka wa 2024.
Anakiri kuwa alinyanyaswa kwa maneno makali katika mitandao ya kijamii baada ya kuvuma.
Baadhi ya mashabiki walimtuhumu kwa kuwa na kiburi wakisema hakufaa kukabiliana na watu waliomrushia matusi na badala yake atulie na kushughulika na tasnia ya muziki.
“Imebidi nikabiliane na mahasimu hawa bila kuogopa,” msanii huyu aliambia Taifa Leo katika mahojiano ya awali.
Aliambia Taifa Leo kuwa alikuwa anapokea jumbe za “Lala mahali pema peponi” pamoja na zile za vitisho alipokuwa kidedea katika ulingo wa muziki mwaka jana.
Ili kupata kinga, aliripoti vitisho hivi katika kituo cha polisi cha Iten na ikanakiliwa katika kitabu cha matukio kwa nambari 20/12/04/23.
‘Atafuta nyota yake’
Baada ya kuvuma, msanii huyu kwa jina halisi, Millicent Jerotich, ufuasi wake ulianza kudidimia mavumbi ya makabiliano mitandaoni yalipotulia.
Kibao chake kilichofanya vizuri mwisho wa mwaka wa 2023 sasa umetazamwa zaidi ya mara milioni 14 kufikia Novemba 19, 2024.
Ni wimbo uliovuna mashabiki wapya na kufufua utazamaji wa nyimbo zake za awali ambazo zilikuwa zimekwama kama vile ‘Tororot’ ambayo imetazamwa zaidi ya mara milioni 1.4.
Marakwet Daughter ana Imani kibao hiki kipya kitamuinua tena kimuziki.
Kufikia sasa, Sherehe Kikwetu (Sisi ni wale), imeonwa kwa angalau mara 16,000 tangu ipakiwe katika mtandao wa YouTube.
Wimbo ambao uliwekwa katika mtandao huo bila video imetazamwa zaidi ya mara 9,400 kufikia Novemba 19, 2024.
“Hongera kwa kuzindua wimbo mkubwa unaofaa msimu wa shamrashamra,” alisifu shabiki mmoja.
“Huu wimbo umenitengenezea siku na imebidi nirudie mara kadhaa kuusikiliza,” shabiki mwingine alisema.