Afya na Jamii

Ndoa husaidia wanaume kufukuza uzee kushinda wanaosalia makapera – Utafiti

Na CECIL ODONGO November 28th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

WANAUME ambao wameoa huwa hawazeeki haraka ikilinganishwa na wale ambao ni makapera, utafiti umebaini.

Utafiti huo uliochapishwa katika jarida la International Social Work ulizamia umuhimu wa ndoa kwa wanaume na wanawake na mchango wake katika ukongwe wao.

Hata hivyo, kwa wanawake haikubainika iwapo maisha ya ndoa yanapunguzia uzee.

Kwenye utafiti huo uliochukua miaka 20, wanaume ambao wana umri wa kati ya miaka 45-85 walishirikishwa na maisha yao kuangaziwa.

Mwonekano wao, afya ya kiakili, mtagusano wao na jamii na umri ni kati ya vigezo ambavyo viliangaziwa.

Kwa ujumla utafiti huo ulionyesha kuwa wanaume ambao walikuwa kwenye ndoa, walikuwa na siha njema, hawakuonekana kutatizika kiakili na licha ya kuwa umri wao ulikuwa umesonga, wengi bado walionekana kuwa vijana.

Wale ambao walikuwa na utulivu kwenye ndoa zao, walionekana wachanga ikilinganishwa na umri wao kutokana na kujitunza vizuri na mahitaji yao kukidhiwa na wake wao.

Ilibainika ndoa tulivu huimarisha afya ya kiakili ya wanaume huku wale ambao ni makapera wakiandamwa na matatizo mbalimbali ya kiakili.

Utafiti huo ulibaini kuwa asilimia 79 ya makapera wapo katika hatari ya kuandamwa na msongo wa mawazo ikilinganishwa na wale ambao wameoa.

Hata hivyo, talaka, mume na mke kutengana, kifo cha mke au mume, huwa na mchango hasi kwenye afya ya mume au mke na husababisha wao kutinga uzeeni haraka kuliko umri wao.

Kwa wanawake, udhabiti wa ndoa si hoja sana kwenye afya yao ya kiakili kwa sababu wengi wao hawaithamini na wapo radhi kuishi hata bila asasi hiyo muhimu katika jamii.

Wanawake wengi huthamini sana kutangamana na marafiki na uhusiano ambao umewaweka kwenye ndoa, hugharimu sana muda wao kwa kushiriki shughuli za nyumbani.