Akili Mali

Uchachushaji kuunda lishe ya mifugo kutumia mifuko ya plastiki

Na LABAAN SHABAAN November 30th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WAKATI wafugaji wa mifugo kama vile ng’ombe wanapitia changamoto ya utoshelevu wa lishe, ubunifu wa kutengeneza na kuhifadhi chakula huhitajika.

Kuna matukio ya uharibifu na hasara ambayo hushuhudiwa baada ya mavuno ya mazao ambayo aghalabu hutumiwa kuunda chakula cha mifugo.

Baadhi ya mimea hiyo ni miwa, mihindi na nyasi mbalimbali ikiwemo napier.

Samuel Kinyanjui Gatimu ni mkulima na mfugaji wa ng’ombe zaidi ya kumi eneo la Ndakaini, Gatanga, Kaunti ya Murang’a.

Bw Gatimu huunda lishe ya kutumiwa kwa muda mrefu kati ya miezi sita na mwaka mmoja almaarafu silage.

Silaji ni aina ya chakula cha mifugo kilichotengenezwa kutoka kwa mazao mabichi ambayo yamehifadhiwa kwa uchachushaji, utaratibu ambao huhakikisha hewa haingii katika mifuko inayohifadhi chakula hicho.

Nyasi ya napier shambani. Picha|Labaan Shabaan

“Mimi sipendi kuweka silaji katika mifuko na kuzika ndani ya ardhi kwa sababu huwa sina uwezo wa kuangalia kama mchakato unaendelea vizuri,” akasema Bw Gatimu akieleza kuwa panya huwa hatari na ikiwa watatoboa mifuko hiyo, chakula kitaharibika.

“Badala ya kuchimbia chini ya udongo, mimi huweka mifuko ya plastiki katika shamba langu ambapo huwa ninatembea mara kwa mara na kuangalia maendeleo yake.”

Mkulima huyu anasema kuwa anapendelea kuchachusha vipande vya nyasi aina ya napier kuunda malisho ya mifugo.

“Unaweza kuviondoa kutoka kwenye mfuko wa plastiki na kuwalisha wanyama wako, na vile vile wanyama wanavipenda kwa sababu ya ladha nzuri,” anasifu.

Mfugaji wa ng’ombe Samuel Kinyanjui Gatimu akiwa shambani mwake eneo la Ndakaini, Gatanga, Kaunti ya Murang’a. Picha|Labaan Shabaan

Bw Gatimu huunda silaji kwa kutumia nyasi, unga wa mahindi na molasi. Baada ya kuvuna nyasi ya napier iliyokomaa, mfugaji huyu huzikatakata kwa mashini na kuanika zikauke kwa siku tatu ili kupunguza kiwango cha maji.

“Weka ndani ya karatasi ya plastiki na uhakikishe hewa haingii. Panya huweza kutoboa, hivyo kuwa makini. Ikiwa utafuata hatua hizi kwa usahihi, unaweza kukaa na silage mwaka mzima,” Bw Gatimu anafafanunua mbinu yake ya kuunda lishe.

Mimea ya mahindi shambani. Hutumika kutengeneza silaji. Picha|Labaan Shabaan

Bw. Gatimu aliendelea: Kama hii niliyo nayo, nimekaa nayo miezi sita. Bora isiingize hewa. Kuwa ukikagua mara kwa mara.”

Kwa kufuata maelekezo haya, pamoja na ushauri wa madaktari wa mifugo, anapata maziwa ya kutosha, lita 25 – 30 kwa ng’ombe kwa siku, kutokana na tiba bora, malisho bora kwa wakati, maji safi ya kutosha, na vyakula vya aina nyingine.

Kwa kufuata maelekezo ya kitaalamu na ushauri wa madaktari wa mifugo, Bw. Gatimu amefanikiwa kupata maziwa ya kutosha, lita 25 hadi 30 kwa ng’ombe kila siku.

Ng’ombe wakiwa zizini katika shamba eneo la Ndakaini, Gatanga, Kaunti ya Murang’a. Picha|Labaan Shabaan

Hii ni kutokana na mchanganyiko wa tiba bora kwa ng’ombe, malisho bora kwa wakati, maji safi ya kutosha, na vyakula vya aina nyingine.

Kila kipengele kina umuhimu wake katika kuhakikisha uzalishaji mzuri wa maziwa.

Tiba bora huhakikisha kuwa ng’ombe wanakuwa na afya nzuri, na hivyo wanakuwa na uwezo mkubwa wa kutoa maziwa.

“Madaktari wa mifugo wanasaidia kugundua na kutibu magonjwa mapema kabla hayajawaathiri ng’ombe na kupunguza uzalishaji wa maziwa,” anasema. “Pia, malisho bora kwa wakati ni muhimu kwani ng’ombe wanahitaji chakula cha kutosha kilicho na virutubisho ili kuendeleza afya zao na kutoa maziwa mengi.”

Mtambo wa kukatakata mazao ya kuunda malisho ya mifugo. Picha|Labaan Shabaan