Sibabaishwi na Matiang'i kupewa mamlaka – Ruto
Na CHARLES WASONGA
NAIBU Rais William Ruto ameonekana kupuuzilia mbali dhana kwamba kupandishwa hadhi kwa Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i ni njama ya kumshushia hadhi.
Kwenye ujumbe katika akaunti yake ya Twitter Alhamisi, Dkt Ruto alikana kuwepo kwa taswira hiyo huku akiunga mkono mabadiliko yaliyotangazwa na Rais Uhuru Kenyatta katika utekelezaji wa miradi ya serikali ya kitaifa kuanzia ngazi za juu hadi mashinani.
“Maafisa wa serikali kuu katika ngazi zote wanapaswa kulainisha utendakazi wao ili uoane na amri iliyotolewa na Rais Uhuru Kenyatta kwa kubuni kamati katika ngazi za kaunti, kanda na kitaifa pamoja na katika baraza la mawaziri,” akasema.
Dkt Ruto alisema mabadiliko hayo yatachangia ufanisi katika utekelezaji wa wa miradi na mipango na kufanikisha mawasiliano yote kuhusu mchakato huo.
Dkt Matiang’i ataongoza kamati ya mawaziri wote katika jukumu lake jipya la kuwa mshirikishi wa miradi yote ya serikali ya kitaifa kutoka ngazi ya kitaifa hadi mashinani, kulingana na amri hiyo.
Lakini baadhi ya wafuasi wa Dkt Ruto, haswa wabunge na maseneta, wamechukulia hatua ya Rais kumwongezea Matiang’i majukumu kama njama ya kumhujumu naibu wake.
Vile vile, imefichuka kwamba baadhi ya wabunge wandani wa Dkt Ruto wanapanga kukutana wiki ijayo kuchambua masuala ibuka katika ulingo wa siasa katika siku za hivi karibuni, kukiwemo kupandishwa hadhi kwa Dkt Matiang’i na athari zake katika ndoto ya Ruto za kutaka kuingia Ikulu mnamo 2022.
“Kama wafuasi wa Naibu Rais, hatutaki kurusha makonde hewani. Sasa tunajipanga upya ili hayo makonde yaelekezwe mahali mwafaka,” akasema Mbunge wa Keiyo Kusini Daniel Rono.
Akaongeza, “Tuliona ni bora tunyamaze kwa sababu hiyo ndiyo mbinu ya kumweka adui gizani ili asijue mipango yako. Mkutano huo ambao umepangwa na kiongozi wa wengi ni muhimu na utakuwa wa manufaa makubwa.”
Alhamisi asubuhi, Dkt Ruto aliongoza mkutano wa viongozi wa Kanisa la Pentecostal Evangelistic Fellowship of Africa katika makao yake rasmi mtaani Karen.
Katika mkutano huo ambao ulidumu kwa saa mbili, Ruto hakuwataja wale wanaodhaniwa kuwa maadui wake wa kisiasa.
Badala yake, alitoa wito kwa viongozi wa kidini kuunga mkono juhudi za serikali za kupambana na ufisadi.