• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 6:50 AM
‘Handisheki’ inavyomfaa Raila

‘Handisheki’ inavyomfaa Raila

Na BENSON MATHEKA

MUAFAKA maarufu kama “handisheki” kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Raila Odinga umeibuka kuwa unaomfaa zaidi kiongozi huyo wa upinzani kuliko wananchi pamoja na wanasiasa wengine.

Kulingana na Rais Kenyatta na Bw Odinga, mwafaka wao ulidhamiria kutuliza siasa na kuunganisha Wakenya ambao wamekuwa wakigawanyika kutokana na misimamo ya kisiasa hasa kuhusu wawili hao.

Lakini imejitokeza kuwa Bw Odinga ndiye anayevuna pakubwa kutokana na muafaka huo huku joto la kisiasa likipanda hasa kuhusu urithi wa urais 2022, na hatari ya kuzuka kwa migawanyiko ya kikabila ambayo wawili hao walisema walitaka kumaliza.

Ushirikiano huo umekita mizizi katika familia zao na wadadisi wanasema Bw Odinga amepata amani na utulivu tofauti na ilivyokuwa alipokuwa akikosoa serikali mara kwa mara.

Familia yake imekuwa karibu sana na ya Rais Kenyatta na duru zinadokeza viongozi hao wamekuwa wakishauriana mara kwa mara faraghani.

Mnamo Jumatano, Seneta Maalum Beth Mugo na ndugu yake Ngengi Muigai, ambao ni binamu wa Rais Kenyatta, walimtembelea Bw Odinga katika ofisi yake Capitol Hill, Nairobi.

Ziara yao ilijiri siku chache baada ya ndugu yake Rais Kenyatta, Bw Muhoho Kenyatta, kuhudhuria ukumbusho ya kifo cha baba ya Bw Odinga, Jaramogi Oginga Odinga nyumbani kwake Bondo, Kaunti ya Siaya.

Bw Muhoho, ambaye hajitokezi sana hadharani hasa kwenye shughuli za kisiasa, alikiri kwamba alimtembelea Bw Odinga kwa sababu ya “handisheki”.

“Mimi sio mwanasiasa, lakini ninapenda maendeleo na nitashikana na Raila ili kuafikia maono ya ustawi kwa Wakenya wote,” Bw Muhoho alisema.

Mapema mwezi huu, familia ya Bw Odinga iliungana na Rais Kenyatta mjini Mombasa kuadhimisha siku ya kuzaliwa kwa kiongozi huyo wa upinzani ambapo walionekana wakijumuika kusakata densi.

Kulingana na Profesa Macharia Munene wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Amerika (USIU), Bw Odinga amenufaika pakubwa na “handisheki” ikiwa ni pamoja na kuteuliwa Mjumbe Maalum wa Muungano wa Afrika AU.

“Cheo hicho ni faida ya muafaka wake na Rais Kenyatta. Kinapandisha hadhi yake barani Afrika na kote ulimwenguni na pia kina manufaa ya kifedha,” Prof Munene aliambia Taifa Leo.

Bw Odinga pia amekuwa akipata taarifa kuhusu taasisi za Serikali, suala ambalo linazua maswali kuhusu anapokea taarifa hizo katika wadhifa upi.

Mfano wa majuzi ni Jumanne wiki jana wakati Afisa Mkuu wa Tume ya Walimu (TSC), Nancy Macharia alipomtembelea Bw Odinga katika ofisi yake kumuarifu jinsi tume inavyoshughulika suala la uhaba wa walimu.

Tofauti na alipokuwa akisumbua serikali kabla ya “handisheki”, Bw Odinga amekuwa akipatiwa heshima ya kiongozi mashuhuri kila anapokwenda huku akisindikizwa na magari ya polisi.

Pia imebainika kuwa makao yake Nairobi, Bondo na Mombasa huwa yako chini ya ulinzi mkali wa polisi.

“Muafaka ulimfaidi Raila kwa namna nyingi pamoja na kumfanya kuwa na shughuli za maana za kufanya kuliko awali,” alisema Prof Munene.

Kulingana na mdadisi wa masuala ya kisiasa Geoffrey Kamwanah, Bw Odinga sasa anafurahia minofu badala ya kumeza mate ilivyokuwa kabla ya muafaka wake na Rais Kenyatta.

“Bw Odinga amekuwa akitumia muafaka kusukuma ajenda zake serikalini. Kwa hakika, amenufaika pakubwa kuliko alipokuwa kwenye baridi la kisiasa,” asema Bw Kamwanah.

Matunda bado kwa wananchi

Lakini Bw Odinga anaporarua minofu ya “handisheki”, kwa upande mwingine kunao wanaohesabu hasara ya mwafaka huo wakiongozwa na Naibu Rais William Ruto.

Tangu mwafaka huo mwaka jana, nyota ya Dkt Ruto kisiasa hasa kuhusu urithi wa urais baada ya Rais Kenyatta kustaafu 2022 imeonekana kudidimia. Hii imetokana na Bw Odinga kusikizwa zaidi na Rais Kenyatta kuliko yeye, suala ambalo limeshusha uhusiano wa karibu uliokuwepo kati ya rais na naibu wake.

Washirika wa Dkt Ruto wamekuwa wakidai kuwa Bw Odinga anatumia mwafaka kujinufaisha kibinafsi hasa kuhusu 2022, suala ambao huenda likazua migawanyiko ya kikabila kati ya wafuasi wa wawili hao.

Chama tawala cha Jubilee pia kimepata pigo kutokana na “handisheki” baada ya mizozo kuibuka ikihusisha kambi zinazounga mkono Dkt Ruto na Bw Odinga, licha ya kuwa kiongozi huyo wa upinzani si mwanachama wa Jubilee.

Wakosoaji wa Bw Odinga walionya mara baada ya mwafaka mnamo Machi 9, 2018 kuwa kiongozi huyo alikuwa na nia ya kuvuruga Jubilee kama alivyofanya awali katika vyama na miungano ya kisiasa.

Wakenya wa kawaida nao wanahisi “handisheki” inanufaisha Bw Odinga na wandani wake kibinafsi hasa baada ya kudhoofika kwa upinzani, hali ambayo imefanya kukosekana kwa ukosoaji kwa serikali, wajibu ambao Bw Odinga alitekeleza kikamilifu kabla ya muafaka.

Badala ya kutetea mwananchi, Bw Odinga sasa anaonekana kuwa mkereketwa wa serikali, ambaye anaunga mkono kila hatua hata zile zinazonyanyasa mwananchi, mfano ikiwa ni ushuru wa VAT ya mafuta mwaka jana.

Lakini kwa upande mwingine, handisheki imesaidia kuwepo kwa utulivu nchini na kupungua kwa uadui uliokuwepo baina ya wafuasi wa Bw Odinga na wa Rais Kenyatta.

Utulivu huu umeleta manufaa ya kiuchumi hasa kwa wafanyibiashara katika jiji la Nairobi ambao awali walitatizwa na maandamano ya mara kwa mara yaliyokuwa yakiitishwa na Bw Odinga. Utalii pia umeinuka.

You can share this post!

Bandari na Sharks ndani ya fainali ya kumenyana na Everton

Waumini wa kanisa la Methodist wajitenga na kanisa kuu

adminleo