HabariKimataifaSiasa

Tanzania: Tundu Lissu akoroga Chadema uchaguzi mkuu ukibisha 2025

Na BOB KARASHANI December 17th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NAIBU mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania – Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) – Bw Tundu Lissu, amethibitisha nia yake ya kupambana na mwenyekiti wa sasa Freeman Mbowe katika uchaguzi ujao wa chama.

Uamuzi wa Bw Lissu huenda usababishwa mgawanyiko  mkubwa katika chama hicho wakati huu kinajaribu kupoza “majeraha” ya kushindwa katika chaguzi za serikali za mitaa mwezi jana.

Chadema ilishindwa vibaya na chama tawala, Chama Cha Mapinduzi (CCM), japo kwa njia ya kutatanisha.

Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe (kushoto), na Bw Lissu wakishangilia na wafuasi wao jijini Dar es Salaam, Tanzania, awali 2023. PICHA | REUTERS

Bw Lissu alitoa tangazo hilo Desemba 12, 2024, siku mbili baada yake na Bw Mbowe kuonekana kuungana na kutangaza kuwa watapigania mageuzi ya kidemokrasia nchini Tanzania katika chaguzi za urais na wabunge zitakazofanyika Oktoba 2025.

Mbowe ameshikilia wadhifa wa mwenyekiti wa Chadema kwa miaka 20. Chama hicho hakijatangaza tarehe kamili ya uchaguzi wa viongozi wake wakuu. Hata hivyo, duru zinasema kuwa huenda zoezi hilo likafanyika katikati mwa mwezi wa Januari 2025.

Hapo Desemba 10, 2024 Bw Mbowe akiandamana na Bw Lissu alisema kuwa mkutano wa kamati kuu uliofanyika wiki jana jijini Dar es Salama uliamua chama kielekeze juhudi zake kupigania katiba mpya na haki katika mfumo wa uchaguzi.

Rais Samia Suluhu wa Tanzania katika hafla ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) jijini Arusha, Tanzania, mwezi Novemba. Uchaguzi mkuu nchini humo ni Oktoba 2025. PICHA | MAKTABA

Hii ni kutokana na chaguzi za Novemba 27, 2024 ambazo Chadema ilidai hazikuendeshwa kwa njia ya haki na ukweli.

Bw Mbowe alisema chama hicho kitajikita katika kampeni hiyo ya kupigania mageuzi baada ya kutendewa hiana na CCM.

Chama tawala CCM kilishinda zaidi ya asilimia 99 ya viti katika ngazi za vijiji, mitaa na kata ndogo; matokeo ambayo yanaakisi yale ya 2019 yaliyoipa ubabe wa kuendelea kutawala siasa za mashinani Tanzania.

Imetafsiriwa na Charles Wasonga