Kimataifa

Trump anapanga kuondoa Amerika katika WHO siku ya kwanza ofisini

Na REUTERS December 24th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WANACHAMA wa timu ya mpito ya urais ya Donald Trump wanapanga Amerika kujiondoa kutoka Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) siku ya kwanza ya muhula wake wa pili, kulingana na mtaalam wa sheria za afya anayefahamu majadiliano hayo.

“Nina habari za kuaminika kwamba anapanga kuiondoa Amerika, labda siku ya kwanza au mapema sana katika utawala wake,” alisema Lawrence Gostin, profesa wa afya ya kimataifa katika Chuo Kikuu cha Georgetown huko Washington na mkurugenzi wa Kituo cha ushirikiano cha WHO kuhusu Sheria Afya Kitaifa na Ulimwenguni.

Gazeti la Financial Times lilikuwa la kwanza kuripoti kuhusu mipango hiyo, likiwataja wataalam wawili. Mtaalam wa pili, mratibu wa zamani wa kukabiliana na COVID-19 katika Ikulu ya White House, Ashish Jha, hakupatikana mara moja kutoa maoni.

Timu ya mpito ya Trump haikujibu mara moja ombi la Reuters la kutoa maoni.

Mpango huo, ambao unaambatana na ukosoaji wa muda mrefu wa Trump wa shirika la Afya Ulinwenguni, unaashiria mabadiliko makubwa katika sera ya afya ya kimataifa ya Amerika na kutenga zaidi Washington kutoka kwa juhudi za kimataifa za kupambana na milipuko.

Trump amewateua wakosoaji kadhaa wa shirika hilo katika nyadhifa za juu zinazohusu afya ya umma, akiwemo Robert F. Kennedy Jr. anayepinga chanjo ambaye atakuwa waziri wa Afya na Huduma za Kibinadamu, ambayo inasimamia mashirika yote makubwa ya afya ya Amerika ikiwa ni pamoja na CDC na FDA.

Trump alianzisha mchakato wa mwaka mzima wa kuondoa Amerika kutoka WHO mnamo 2020 lakini miezi sita baadaye mrithi wake, Rais Joe Biden, alibatilisha uamuzi huo.

Trump amedai kuwa shirika hilo lilishindwa kuiwajibisha China kwa kuenea mapema kwa COVID-19. Amerudia kutaja WHO kuwa kibaraka wa China na kuapa kuelekeza michango ya Amerika kwa mipango ya afya ya ndani.

Msemaji wa WHO alikataa kutoa maoni yake moja kwa moja lakini alielekeza Reuters kwa maoni ya Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus katika mkutano na waandishi wa habari mnamo Desemba 10 ambapo aliulizwa ikiwa alikuwa na wasiwasi kwamba utawala wa Trump utajiondoa kutoka kwa shirika hilo.

Tedros alisema wakati huo kwamba WHO ilihitaji kupatia Amerika wakati na nafasi ya mpito. Pia alionyesha imani kwamba serikali zitaweza kukamilisha makubaliano kuhusu milipuko ifikapo Mei 2025.

Wakosoaji wanaonya kuwa kujiondoa kwa Amerika kunaweza kudhoofisha ufuatiliaji wa magonjwa ulimwenguni na mifumo ya kukabiliana na dharura.

“Amerika itapoteza ushawishi na nguvu katika afya ya kimataifa na China itajaza nafasi itakayoacha. Siwezi kufikiria ulimwengu usio na WHO imara. Lakini kujiondoa kwa Amerika kutadhoofisha sana shirika hilo,” Gostin alisema.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA