Kimataifa

Aliyekuwa rais wa 39 wa Amerika Jimmy Carter afariki akiwa na umri wa miaka 100

Na MASHIRIKA December 30th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

JIMMY Carter, mkulima mwenye bidii wa Georgia ambaye akiwa rais wa 39 wa Amerika alipambana na uchumi mbaya na mgogoro wa mateka wa Iran lakini akaleta amani kati ya Israeli na Misri na baadaye akapokea Tuzo ya Amani ya Nobel kwa kazi yake ya kibinadamu, alifariki dunia nyumbani kwake huko Plains, Georgia, Jumapili.

Alikuwa na umri wa miaka 100.

Rais wa Amerika Joe Biden alitangaza kwamba Januari 9 itakuwa siku ya kitaifa ya kuomboleza Carter kote Amerika.

“Ninatoa wito kwa watu wa Amerika kukusanyika siku hiyo katika maeneo yao ya ibada, kutoa heshima kwa kumbukumbu ya Rais James Earl Carter,” Biden alisema.

Carter, mwanademokrasia, aliingia mamlakani Januari 1977 baada ya kumshinda Rais wa Republican Gerald Ford katika uchaguzi wa 1976.

Urais wake wa muhula mmoja uliwekwa alama na viwango vya juu vya makubaliano ya Camp David mwaka wa 1978 kati ya Israeli na Misri, na kuleta utulivu katika Mashariki ya Kati.

Lakini pia ulikumbwa na kudorora lwa uchumi, kutopendwa na watu wengi na mzozo wa mateka wa Iran ambao ulitanda siku zake za mwisho 444 madarakani. Carter aligombea muhula wa pili mwaka wa 1980 lakini aliondolewa ofisini kwa kishindo huku wapiga kura wakimkumbatia mpinzani wa chama cha Republican Ronald Reagan, mwigizaji wa zamani wa sinema na gavana wa California.

Carter ameishi muda mrefu zaidi kuliko rais yeyote wa Amerika, baada ya kuondoka Ikulu ya White House, alipata sifa kama mfadhili aliyejitolea.

Alionekana sana kama rais wa zamani bora kuliko alivyokuwa akiwa rais – hadhi ambayo aliikubali kwa urahisi.

Viongozi wa dunia na marais wa zamani wa Amerika walimtaja kama mtu waliyemsifu kuwa mwenye huruma, mnyenyekevu na aliyejitolea kuleta amani Mashariki ya Kati.

“Jukumu lake kubwa katika kufikia makubaliano ya amani kati ya Misri na Israel litaendelea kubaki katika kumbukumbu za historia,” Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi alisema katika chapisho kwenye X.

Kituo cha Carter kilisema kutakuwa na maadhimisho ya umma huko Atlanta na Washington. Matukio haya yatafuatiwa na sala ya kibinafsi huko Plains, ilisema.

Mipango ya mwisho ya mazishi ya rais huyo wa zamani bado haijatolewa, kulingana na kituo hicho.

Katika miaka ya hivi majuzi, Carter alipata matatizo kadhaa ya kiafya ikiwa ni pamoja na saratani ambayo ilienea kwenye ini na ubongo wake.

Mkewe, Rosalynn Carter, alikufa mnamo Novemba 19, 2023, akiwa na umri wa miaka 96. Alionekana dhaifu alipohudhuria mazishi yake katika kiti cha magurudumu.

Carter aliondoka afisi bila umaarufu mkubwa lakini alifanya kazi kwa bidii kwa miongo kadhaa kuhusu masuala ya kibinadamu.

Alitunukiwa Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka wa 2002 kwa kutambua “juhudi zake  za kutafuta amani kwa migogoro ya kimataifa, kuendeleza demokrasia na haki za binadamu, na kukuza maendeleo ya kiuchumi na kijamii.”

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA