Mashairi

MASHAIRI YA JUMAMOSI: Siutaki uke wenza

January 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

Mume wangu nakupenda, tangu tulipokutana,
Na mapenzi yakatanda, mpaka tukaoana,
Mengi nayo tumetenda, tumezidi kupendana,
Simtaki mke mwenza, mume wangu nakupenda.

Nimekuwa nikipika, huku ukinisifia,
Chakula changu chalika, mpaka wafurahia,
Sasa nini unataka, huwezi kuniambia,
Simtaki mke mwenza, mume wangu nakupenda.

Juzijuzi nimeona, meanza kubadilika,
Unawapenda vichuna, kwa sasa unawataka,
Wawaona wa maana, hauchoki kuwasaka,
Simtaki mke mwenza, mume wangu nakupenda.

Hukumbuki kanisani, ahadi uliyonipa,
Wakiona waumini, hadi busu nikakupa,
Pete nalo kidoleni, kukulinda nikaapa,
Simtaki mke mwenza, mume wangu nakupenda.

Tumetoka mbali sana, hivyo basi fikiria,
Jinsi tulivyopambana, hadi tumeendelea,
Haja gani kunikana, pasipo kuniambia,
Simtaki mke mwenza, mume wangu nakupenda.

Watoto tumewapata, angalau wako sita,
Mitaani nikipita, ninaitwa mamasita,
Sitaki nami matata, vipusa unaofwata,
Simtaki mke mwenza, mume wangu nakupenda.

Chunga hawa wasichana, pesa watazimaliza,
Utafakari kwa kina, hawawezi kukusaza,
Familia ni maana, sauti yangu napaza,
Simtaki mke mwenza, mume wangu nakupenda.

Mwisho hapa ninafika, na uzuri nimesema,
Kwa ukweli nimechoka, kila siku kutazama,
Sitaki kuhangaika, nikishinda kulalama,
Simtaki mke mwenza, mume wangu nakupenda.
MALENGA KITONGOJINI,
 LIONEL ASENA VIDONYI.
TONGAREN, NDALU

Shule zimefunguliwa
Na muhula umeanza, wanafunzi pulikani,
Wavyele wamewatunza, siku zote likizoni,
Na sasa ni kujifunza, na mwalimu darasani,
Shule zimefunguliwa, ni wakati wa kusoma.

Ni wakati wa kusoma, na kuonyesha nidhamu,
Utukutu wako koma, walimuo waheshimu,
Anayekataa pema, pabaya ‘tajilaumu,
Shule zimefunguliwa, ni wakati wa kusoma.

Vitabu vyako uvisome, na kazizo kumaliza,
Na uzembe uukome, unaposhindwa uliza,
Ni shariti uiname, sikiliza nakujuza,
Shule zimefunguliwa, ni wakati wa kusoma.

Michezo nayo shiriki, ukitafute kipawa,
Ukipenda cheza hoki, au riadha ni sawa,
Mashindano ‘tashiriki, duniani ‘tasifiwa,
Shule zimefunguliwa, ni wakati wa kusoma.

Yaghani na mashairi, kwa mahadhi mbalimbali,
Ukipenda yakariri, vyema na kwa kila hali,
Vipaji vyote vizuri, vitie kote makali,
Shule zimefunguliwa, ni wakati wa kusoma.

Na usafi zingatia, wa mwili na mazingira,
Kwa maji safi ogea, upendeze uwe bora,
Epuka nakuambia, uchafu sana hukera,
Shule zimefunguliwa, ni wakati wa kusoma.

Kaditama ninakoma, hapa ndipo kituoni,
Ninakutakia mema, ukiwa hapa shuleni,
Mimi ni mwalimu Juma, mkuu wa shule hini,
Shule zimefunguliwa, ni wakati wa kusoma.
CHRISTOPHER MUSA KALUNDA
 MALENGA MWEPESI,
 KABARNET, BARINGO

Utamwita baba?
Umuogope adui, amtusiye babayo,
Ufyosi yake nishai, ana njama mtu huyo,
Muogope ni mbuai, itwaa kauli hiyo,
Atamuuwa si bui, kisha aowe mamayo,

Utamwona na saruni, kiunoni kajifunga,
Angiye nayo chumbani, mwa babayo akifunga,
Umuone hayawani, ila ugwe auunga,
Wakufate mgongoni, wanuna awatunga.
RAMADHAN ABDALLAH SAVONGE,
“KIVUMANZI”
MOMBASA, KENYA

Kengele sasa yalia!
Kengele tena yalia, inatuita shuleni,
Ni tafauti sikia, na ya ng’omba machungani,
Yatuita kukimbia, tuingie darasani,
Kwamba turudi shuleni, kisomo kujipatia,

Siri ipo nakwambia, wana tuwapo shuleni,
Walimu kuzingatia, nayo makini somoni,
Kwa ari kukaribia, pa fumbo wafumbueni,
Kwamba turudi shuleni, kisomo kujipatia,

Watundu kuwakimbia, wazuao tafrani,
Mbali nao kupitia, situtie matatani,
Mbumbu kukaribia, tatutia mashakani,
Kwamba turudi shuleni, kisomo kujipatia,

Iwapo sijasikia, mwalimu ataka nini,
Mkono nitaenua, niombe aniauni,
Lugha safi kutumia, miko na utamaduni,
Kwamba turudi shuleni, kisomo kujipatia,

Wapo wanaochukia, mazingira ya shuleni,
Hasidi tunavyojua, sababu hana hanani,
Siku yaja kujutia, si leo pale mbeleni,
Kwamba turudi shuleni, kisomo kujipatia,

Muda tutakadiria, kutumia kwa makini,
Jiangalie kisia, mwisho utavuna nini,
Usiwe unasinzia, kukoroma darasani,
Kwamba turudi shuleni, kisomo kujipatia,

Wino wanikaukia, Malenga wa migombani,
Najua menisikia, niloyatoa kinywani,
Mwanafunzi zingatia, wa kutwa au wa bweni,
Kwamba turudi shuleni, kisomo kujipatia,
NYAGEMI NYAMWARO MABUKAH.
“MALENGA WA MIGOMBANI”
MIGOMBA YA ZIWA KUU

Andaeni wanafunzi
Jukwaani nimefika, satua meipatani,
Naanza huu mwaka, waadhi kuwapani,
Sherehe zilowaka, hatimaye mekwishani,
Andaeni wanafunzi, warudipo shuleni.

Msimu Krisimasi, darahimu hutumika,
Januari pia mosi, dhifa nyingi hufanyika,
Zitumike tu kiasi, karo sije adimika,
Andaeni wanafunzi, warudipo shuleni.

Elimu ni laazizi, sitanie mwafulani,
Hupenya yake mizizi, matundake matamuni,
Elimu ni lainizi, hutiliwa maanani,
Andaeni wanafunzi, warudipo shuleni.

Mabuku yaandaliwe, wosia pia wapewe,
Maadili yapaliwe, wahimizwe waelewe,
Matukano wasitupiwe, kwa upendo waelezewe,
Andaeni wanafunzi, warudipo shuleni.

Ukurasa wafungue, waanze kwa kishindo,
Razini wazifungue, waukaze wao mwendo,
Hamu na ghamu tuwatie, wakasome kwa upendo,
Andaeni wanafunzi, warudipo shuleni.

JESSE CHEGE MWANGI
 (MALENGA MZALENDO)
SHULE YA LORD EGERTON, NJORO
NAKURU

Kiti chawaka moto
Wembe anapolilia, usimnyime mtoto,
Mbio ulikimbilia, kwenye njia za mkato,
Bahati ukalalia, kupawa kubwa kipato,
Kiti ulikililia, sasa kinawaka moto.

Fitina kumtilia, ukawa nd’o mwenye kito,
Patupu kaambulia, kwenye cheche zako nzito,
Bosi kakukubalia, kukuongeza kipato,
Kiti ulikililia, sasa kinawaka moto.

Kwa machozi alilia, kutoka kama mtoto,
Ni pekee familia, waliohisi uzito,
Rafiki wakatulia, kama wako kwenye ndoto,
Kiti ulikililia, sasa kinawaka moto.

Alipo kikwamilia, mkaudondosha mto,
Pagumu kupakalia, mkaanza mchakato,
Hana cha kumsalia, mtume kwenye mazito,
Kiti ulikililia, sasa kinawaka moto.

Kigoda kukikalia, kinakuchoma kwa moto,
Vizuri umevalia, moyo waungua joto,
Ni kwa nini unalia, kwenye hii rangaito,
Kiti ulikililia, sasa kinawaka moto.

Hutaki kuachilia, japo upo kwa majuto,
Kwenye Mia asilia, nafusi yawaka moto,
Huwezi kukikalia, umezidi mchecheto,
Kiti ulikililia, sasa kinawaka moto.
EDISON WANGA
SON BIN EDI, MWANA WA MAMBASA
MOMBASA