Sekta ya afya inaugua na inahitaji matibabu kamili
MATUKIO yanayochipuka nchini kila uchao yamezua maswali na kuwaacha wengi wakiduwaa iwapo serikali imeshindwa kujipanga au inahujumiwa tu na mahasimu wake waliopania kuisawiri vibaya.
Licha ya kujizatiti kuchora taswira kwamba hali ni shwari, ni bayana kuwa mambo mengi yanakwenda mrama miaka mitatu tangu serikali mpya ilipochukua usukani.
Iwapo si wafanyabiashara wanaokadiria hasara, ni madaktari na wauguzi wanaobeba mabango barabarani kudai ujira wao.
Shuleni nako hakukaliki baada ya kufunguliwa majuzi huku walimu, wanafunzi na wazazi wakigubikwa na sintofahamu.
Ripoti mpya ya mdhibiti bajeti iliyotolewa majuzi iliashiria utekelezaji duni wa miradi ya maendeleo katika asasi zote za kiserikali.
Siku chache baadaye, Dkt Peter Mbae, mkuu wa utekelezaji miradi na mipango katika uongozi wa Rais William Ruto, alijiuzulu miezi sita tu baada ya kuteuliwa Juni mwaka jana.
Mbae aliyesimamia utoaji huduma za serikali kwa lengo la kufuatilia utekelezaji wa ajenda ya Bottom Up, ya Dkt Ruto, alijiuzulu akitaja masuala ambayo hayajasuluhishwa yaliyotatiza utendakazi wake, hali inayoashiria mambo si shwari.
Sekta ya afya ndiyo iliyoathirika zaidi hasa baada ya kukabiliwa na kipindi kigumu mwaka uliopita kutokana na mageuzi yaliyoathiri bima ya afya ya NHIF.
Hata kabla ya kupata afueni kutokana na masaibu waliyopita mwaka jana, mamilioni ya Wakenya sasa wamo hatarini huku taifa likikabiliwa na ukosefu wa vifaa muhimu vya matibabu.
Hospitali za umma na za kibinafsi hazina dawa muhimu za kutibu HIV wala vifaa vya kufanyia vipimo vya virusi hivyo baada ya kumalizika katika wa msimu wa Krismasi mwaka jana.
Hali hii inatishia kuhujumu juhudi za kupiga vita virusi hivyo ambazo zimefanikisha kupunguza maambukizi ya HIV.
Isitoshe, mustakabali wa watoto wanaozaliwa nchini unaning’nia hatarini huku taifa likikabiliwa na ukosefu wa chanjo muhimu za watoto wachanga.
Chanjo ya BCG husaidia kuwakinga watoto wachanga kutokana na aina sugu ya kifua kikuu na homa ya uti wa mgongo.
Masaibu haya yanajitokeza wakati suala la kujifungua kwa kina mama limegeuka jinamizi huku utata ukigubika bima ya linda mama iliyotegemewa na maelfu ya wanawake.
Wanawake zaidi ya 50 na watoto wao wachanga walizuiliwa kwa miezi kadhaa katika hospitali ya Thika Level 5 baada ya kushindwa kulipa bili ya kujifungua.
Taswira inayojitokeza kuhusu sekta ya afya nchini ni ya kukatiza tamaa na huenda ikasababisha athari kuu iwapo haitashughulikiwa kwa dharura.