AK yaonya ‘wataalamu’ wa kubadilisha umri wa wanariadha
RAIS wa Shirikisho la Riadha Kenya (AK) Jackson Tuwei ameonya makocha, walimu na wazazi dhidi ya kusaidia wanariadha wa humu nchini kudanganya miaka.
Tuwei amefichua kuwa kuna wanariadha kadhaa wanachunguzwa kwa kushiriki mbio za chipukizi kwa kudanganya umri.
Ameonya kuwa hatua hiyo ya kudanganya miaka itakuja kuumiza Kenya hapo mbele.
Tuwei ameongeza kuwa wazazi, walimu ama makocha wamekuwa “wataalamu” wa kubadilisha stakabadhi za kuzaliwa na vitambulisho za wanariadha ili kupunguza umri wao na kuwawezesha kushiriki mashindano ya chipukizi.
“Tutakunyaka tu hata kama ulidanganya umri ukishiriki mbio za chipukizi. Tuna majina mengi tunachunguza wanaoingia vitengo vya watu wazima kutoka chipukizi. Tutaanika majina yao hivi karibuni,” akasema Tuwei na kuwataka wanariadha kuwa waaminifu na pia kukoma udanganyifu huo.
“Hatutaki kudanganya ulimwengu mzima na matokeo mazuri kupitia udanganyifu wa umri,” akasema naibu huyo wa rais wa Shirikisho la Riadha Duniani.
Imetafsiriwa na Geoffrey Anene