Makala

Wagonjwa watatizika Hospitali ya Mama Margaret Uhuru ikihamishwa

Na KEVIN CHERUIYOT January 29th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KUHAMISHWA kwa Hospitali ya Mama Margaret Uhuru hadi Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta kumewasababishia wagonjwa mahangaiko tele wakilazimika kusaka matibabu katika vituo vingine.

Hospitali hiyo ilikuwa ikiwahadumia watu wenye mapato ya chini ambao walikuwa wakiishi mitaa ya Kariobangi Kaskazini, Kariobangi Kusini na Korogocho.

Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja alikuwa mstari wa mbele kumshawishi Rais William Ruto ili hospitali hiyo iliyokuwa na shughuli nyingi ihamishwe hadi KNH.

Taifa Leo ilizuru hospitali ambayo sasa inakaa kama mahame huku wanaoishi kwenye mitaa ya mabanda waliokuwa wakinufaikia huduma za matibabu wakisema uamuzi wa kuihamisha imekuwa pigo kwao.

Majengo mawili ya kisasa ya hospitali hiyo ambayo ingekuwa kwenye kiwango cha Level 6 bad hayatumiki wala hakuna dalili zozote kuwa wagonjwa wanahudumiwa kama zamani.

Hospitali hiyo ina vitanda 400 vya kuwalaza wagonjwa na sehemu kubwa ya maegesho ambayo imesalia mahame. Wodi za kulaza wagonjwa pamoja na sehemu ya kufanya upasuaji nazo hazitumiki.

Biashara za maeneo ya karibu na hospitali ambazo zilikuwa zimeanza kunoga sasa hazipo tena kutokana na uhamisho huo.

Afisa Mkuu wa Hospitali ya Mama Margaret Uhuru Martin Wafula hakupokea simu kutoa maelezo kuhusu hospitali hiyo kutofanya kazi na iwapo itarejelea hadhi yake ya zamani.

Hata hivyo, Dkt Meli Kimaiyo, supritendanti wa hospitali hiyo alisema asilimia 60 za huduma zinaendelea kama kawaida japo bado wanafanyia kazi maeneo mengine.

Kwa sasa hospitali hiyo imekuwa ikiwashughulikia tu wagonjwa wanaokuja kutibiwa kisha kurejea makwao huku baadhi ya wanaougua wakielekezwa wapokee huduma za kimatibabu kwenye Hospitali ya Mama Lucy Kibaki.