Dimba

Refa aliyeonea Arsenal aaibika kadi nyekundu aliyomzaba Myles Lewis Skelly ikifutwa

Na LONDON, UINGEREZA January 29th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KADI nyekundu aliyopewa kinda Myles Lewis-Skelly mwishoni mwa wiki imepinduliwa baada ya Arsenal kushinda kesi ya rufaa mbele ya Shirikisho la Soka nchini Uingereza (FA).

Kijana huyo mwenye umri wa miaka 18 alipewa kadi hiyo Jumamosi wakati wa mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza baina ya Arsenal na Wolves katika mechi ngumu ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ambayo vijana wa Mikel Arteta waliibuka na ushindi wa 1-0.

Kadi hiyo, iliyotolewa na refa Michael Oliver, ya kumfungia chipukizi huyo nje ya mechi tatu mfululizo iliondolewa baada ya kitengo cha tume huru ya FA kuchunguza na kutoa uamuzi.

“Tumefurahia haki imetendeka,” kocha Mikel Arteta alisema usiku wa kuamkia jana alipokuwa akiandaa kikosi chake kucheza na Girona jana usiku katika mechi ya mwisho ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya (UCL).

“Klabu imewasilisha ushahidi wa kutosha na kujitetea vilivyo dhidi ya hatua ya mwamuzi, na tunashukuru waliohusika kwa kufanya uamuzi kwa haraka ambao ni nafuu kwa timu nzima,” aliongeza.

Lewis-Skelly alionyeshwa kadi hiyo baada ya kumchezea ngware Matt Doherty, kosa ambalo mwamuzi Oliver alichukulia kuwa kubwa.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mechi ya UCL, Arteta alisema tabia ya kushambulia marefa kupitia mitandao ya kijamii haifai. Tabia hii alisema, “Inawaweka waathiriwa katika hali ngumu. Tafadhalini tujiepushe.”

Alipoulizwa iwapo alikuwa akilenga mashabiki wa klabu yake, Arteta alisema: “Ni kwa kila mtu katika soka, haifai kukubaliwa kamwe. Hatutaipenda, hatuhitaji kwa sababu inaharibu jina zuri la spoti.”

Kadhalika kocha huyo ambaye takwimu zinaonyesha ameipa Arsenal kadi nyingi (8) nyekundu kuliko timu nyingine yoyote ile katika EPL, alitaka sheria ziwekwe kukabili wanaotoa matusi kupitia mitandao ya jamii, huku akiongeza, kuna sheria zilizowekwa lakini hazijasaidia popote.”

Doherty alikabiliwa akiwa nje kidogo tu ya lango la Wolves alipokuwa akipenya wanasoka wa Arsenal kwa lengo la kufunga angetatizika kufikia lango la wapinzani hao kwani lilikuwa mbali.

Kwenye mechi hiyo iliyochezewa Molineux Stadium, wenyeji vilevile walipunguzwa na kubakia wachezaji 10 baada ya Joao Gomez kupigwa kadi nyekundu dakika ya 70, kabla ya beki nguvu mpya, Riccardo Calafiori kufunga bao la ushindi dakika nne baadaye.

Juma lililopita, kijana wa umri wa miaka 17 alitiwa mbaroni kutokanana na madai ya kumtusi mshambuliaji Kai Havertz wa Arsenal kupitia kwa mtandao wa kijamii, pamoja na mkewe baada ya klabu hiyo kushindwa na Manchester United katika mechi ya FA Cup.

Mbali na hayo, maafisa wa polisi wanaendelea kuchunguza madai ya vitisho kutoka kwa mashabiki wa Arsenal wanaozidi kumwaandama refa huyo, wakidai aliwaonea.

Katika mechi za wikendi za EPL, Oliver ameratibiwa kuchezesha pambanpo kati ya Ipswich na Southampton, Jumamosi.

Hatua hiyo ya kumpeleka maeneo ya Portman Road kuchezea mechi hiyo inamaanisha hatakuwa usukani wakati wa pambano kati ya Arsenal na Manchester City ugani Emirates, ambayo imepewa Peter Bankes.

Baadaye, Oliver atasimamia Merseyside derby kati ya Everton na Liverpool ugani Goodson Parl hapo Februari 5.