Wakazi washambulia washukiwa wa Mungiki, waua wawili
WAKAZI wa Kaunti ya Kirinyaga sasa wameanza kuwakabili watu wanaoshukiwa kuwa wanachama wa kundi haramu la Mungiki.
Mnnamo Jumatano, Januari 29, 2025 wakazi hao waliojawa na hasira waliwakabili washukiwa wawili wa Munguki na kuwakatakata.
Shambulio hilo lilitokea katika shamba la Ngariama Kusini katika Eneo Bunge la Mwea ambapo walivamia ekari 28,000 za ardhi na kuteketeza nyumba saba za washukiwa hao.
Baadhi ya washiriki wa kundi hilo miongoni mwao mwanamke mmoja alifanikiwa kutoroka akiwa na majeraha wakati wa makabiliano ya alasiri ambalo lilivutia umakini wa maafisa wakuu wa usalama wa klaunti hiyo.
Wakazi hao walivamia nyumba za washukiwa hao wakiwashutumu kwa kuwahangaisha wananchi.
Hata hivyo, zaidi ya washukiwa 100 wa Mungiki walizidiwa nguvu na kupigwa vibaya.
Hatua hiyo ilichukuliwa kama njia ya kutoa onyo kali kwa watu wanaohusika na kundi hilo.
Polisi walifika muda mfupi baada ya shambulio hilo na kurejesha utulivu na kuondoa miili katika eneo la tukio na kuipeleka katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya rufaa ya Kerugoya.
Wakazi hao walilalamika kwamba washukiwa hao walivamia eneo hilo mwaka jana na kuanza kunyakua sehemu zao za ardhi kwa nguvu.
Pia wanadaiwa kuwaibia wakazi hao pesa na kuchukua mifugo yao.
“Hawa watu wamekuwa wakituhangaisha, tumesema imetosha,” mkazi mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema.
Wakazi walisema wahusika ni watu wasio na huruma kwani hata wanafanya shughuli zao za kilimo kuwa ngumu.
“Wakulima wanatozwa ada fulani. Kutokana na ada kubwa wanaotozwa, wameacha kulima na hili ni jambo ambalo hatuwezi kuruhusu liendelee,” akasema Bw Mugo Kathiaku.
Mkuu wa polisi katika Kaunti Ndogo ya Mashariki ya Mwea Mohammed Jarso alieleza jinsi kikosi cha usalama kilitembelea eneo hilo kutathmini hali ilivyo.
“Ni kweli watu wawili ambao wakazi hao wanadai kuwa ni Mungiki wameuawa kwa kukatwakatwa na nyumba saba kuteketezwa,” alisema Bw Jarso.
Alisema mzozo huo mbaya kati ya wakazi hao na washukiwa hao ulichochewa na mgogoro wa ardhi katika na kuongeza kuwa suala hilo linachunguzwa.
“Wakazi wanahoji kuwa kikundi cha watu wanaoishi katika eneo hilo wananyakua ardhi yao na kama timu ya usalama tunataka kubaini ukweli wa jambo hilo,” alisema.
Aliwaonya wakazi hao dhidi ya kujichukulia sheria mkononi, huku akiwakumbusha kuwa washukiwa walitakiwa kufikishwa katika kituo cha polisi ili wahojiwe na kufunguliwa mashitaka lakini si kuchukua sheria mkononi.