Michezo

Voliboli: GSU walivyopepeta Kenya Prisons kwa marungu uwanjani Nyayo

Na JOHN KIMWERE February 2nd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

VIGOGO wa voliboli nchini Kenya Prisons waliona siku ndefu wakifurushwa na maafande wenzao General Service Unit (GSU) katika mechi za duru ya tatu ya Ligi Kuu (KVF), Jumamosi.

GSU walionyesha wao uweledi wao kwa kufinya Kenya Prisons seti 3-2 katika mechi ya kukata na shoka uwanjani Nyayo, Nairobi.

GSU ya kocha Gideon Tarus ilibeba seti ya kwanza kwa alama 25-19. Hata hivyo, Prisons inayonolewa na Dennis Mokua ilizinduka na kuonyesha ustadi ambao umewazolea taji la ligi mara mbili mfululizo, kwa kushinda seti ya pili na tatu alama 25-20 na 25-23 mtawalia.

Lakini GSU ilirejea dimbani kwa kishindo na kubeba seti mbili za mwisho kwa alama za 25-11 na 15-13 mtawalia.

Kombora la Josephat Kirwa (kulia) wa Kenya Prisons lazimwa na Shadrack Misiko (kushoto) wa GSU uwanjani Nyayo, Jumamosi. PICHA | SILA KIPLAGAT

“Imekuwa mechi ngumu mbele ya mahasimu wetu hawa wa tangu jadi. Tumekubali yaishe kwa leo,” alisema kocha Mokua wa Kenya Prisons na kuongeza kuwa bado wataendelea kupigania taji hilo.

Mwenzake wa GSU, Tarus, alisema wana hamu kubwa ya kubeba ligi mara ya sita.

“Hatuna muda wa kupumua. Tunataka kushusha wembe uo huo katika mechi zijazo ili tufuzu kwa awamu ya fainali na kisha tunyanyue taji,” akaeleza.

Katika matokeo mengine, wanamisitu wa Kenya Forest Service (KFS) walirarua Kenya Airforce Police Unit (KAPU) kwa seti 3-0 za alama 25-17, 29-27 na 25-22 kwenye mechi ambayo pia ilishuhudia ushindani wa kufa mtu.

Mamlaka ya Kusimamia Bandari za Kenya (KPA) ikanyuka Kenya Prisons Riftvalley kwa seti 3-0 za alama 27-17, 27-25 na 25-14 ikicheza kwa ari dhidi ya wakali hao wa kutoka eneo la Bonde la Ufa.

KPA iliandikisha ushindi huo baada ya kucharaza Kenya Prisons Nairobi kwa seti 3-0 siku iliyotangulia.

“Ninapongeza wachezaji kwa kuendeleza mtindo wetu wa kutoa dozi kali kwa wapinzani,” alideka kocha James Ontere wa KPA na kuongeza kuwa wanafahamu hakuna mteremko katika kupigania taji la msimu huu.

Bonfentry Mkekhe (kushoto) wa GSU afyatua shuti dhidi ya wachezaji wa Kenya Army, Eugene Ochieng (jezi 12) na Andrew Kipyego (kulia), Jumapili. PICHA | CHRIS OMOLLO

Nayo KDF ilisajili ufanisi wa seti 3-0 dhidi ya Kenya Prisons Nairobi. Wanajeshi hao wa kocha Elisha Aliwa walizoa ushindi wa alama 25-22, 25-20 na 25-18.

“Tumekaa kibabe kwenye kampeni zetu licha ya kupokea ushindani mkali kutoka kwa wapinzani wetu,” alisema Aliwa mwenye imani tele kwamba wakiendelea na fomu hiyo ya ushindi ana imani watafuzu kwa duru ya fainali msimu huu.

Trailblazers ilidondosha mechi ya pili mfululizo ilipolala seti 3-2 mikononi mwa Kenya Prisons Western. Ushindi huo wa Kenya Prisons Western ulikuwa wa alama za 19-25, 25-19, 25-21, 21-25 na 16-14. Siku iliyotangulia Trailblazers ilikuwa imepokezwa kichapo cha seti 3-2 na Kenya Prisons Ritfvalley.

Nao wanajeshi wa Kenya Army walisajili ufanisi wa seti 3-1 (21-25, 25-16, 25-17 na 25-21) dhidi ya Shirika la Kitaifa la Huduma za Vijana (NYS).