Hofu wakazi wanauziwa nyama ya punda baada ya vichwa 31 kupatikana Embu
PUNDA 31 ambao wanaaminika waliibwa walipatikana eneo la Makutano, Kaunti ya Embu na kuibua madai kuwa wakazi huenda walikuwa wakila nyama ya punda bila kujua.
Polisi na maafisa wa afya ya umma walivamia boma ya mmiliki mmoja wa buchari Jumamosi na wakashtuka kupata nyama ya punda ikiandaliwa kusafirishwa maeneo mbalimbali.
Maafisa hao walivamia boma hilo baada ya kufahamishwa na umma.
“Mfanyabiashara huyo alikuwa amebadilisha boma lake kuwa kichinjo na tuliwapata punda wakichinjwa ishara kuwa nyama yake imekuwa ikiuzwa,” akasema Mkazi Josphat Maina.
Mashahidi walisema punda hao walikuwa wengi na huenda walikuwa wameibwa.
“Nyumbani kwake tulihesabu vichwa 31 vya punda ambavyo vilikuwa vimetapakaa kote,” akasema Bi Milka Ndung’u.
Wakati wa uvamizi huo, mmiliki wa boma hilo na wafanyakazi wake 10 walifanikiwa kuhepa hadi kichaka cha karibu.
Afisa wa Afya ya Umma wa Mwea Rachel Nyambura alisema nyama hiyo haikuwa imekaguliwa na itatupwa.
“Ni kweli tulipata vichwa 31 vya punda kwenye boma hilo. Tunashuku walikuwa wakipanga kusafirisha nyama hiyo kabla tuwafumanie. Wakazi nao walisema biashara ya nyama ya punda imenoga sana katika eneo hilo, baadhi wakilalamika kuwa ulaji wa nyama hiyo unahatarisha maisha yao.
Kamanda wa Polisi wa Mwea Willy Simba alisema kuwa hawatapumua hadi pale wale ambao wamekuwa wakifanya biashara ya kuuza nyama ya punda wamekamatwa na kushtakiwa.