Wadukuzi wezi wa benki 130 wasakwa Kenya
Na PETER MBURU
IDARA ya DCI Jumatano ilichapisha majina ya watu 130 ambao wanawindwa na polisi, kwa makosa ya kudukua mitambo ya benki.
Kupitia akaunti zake za mitandao ya kijamii na kurasa saba za magazeti ya humu nchini, idara hiyo ilichapisha majina, sura na nambari za vitambulisho za washukiwa hao, huku ikiwataka watu kupiga ripoti kwa polisi wanapowaona.
Wachunguzi hao wa makosa ya jinai aidha walitoa nambari za simu ambazo watu wanaweza kuripoti kwa kupiga simu ama kutuma jumbe fupi.
“Watu hawa wanatakikana kuhusiana na wizi wa kielektroniki kwa kudukua mitambo ya benki,” kurasa hizo zikasoma juu.
Idara ya DCI aidha ilisema kuwa ilipokea amri kutoka mahakama za Kiambu na Milimani kuwakamata washukiwa hao.
“Washukiwa walioorodheshwa hapa wanatakikana na Idara ya Uchunguzi wa Jinai kulingana na amri za korti za Mahakama za Kiambu na Milimani zilizotolewa Januari 24, 2019,” idara hiyo aidha ikasema.
Kati ya washukiwa hao 130, ni mmoja tu ambaye picha yake haikuchapishwa, Alex Fondo Chea. Orodha hiyo vilevile ina wanawake 30, kati ya washukiwa hao 130.
“Mtu yeyote aliye na habari ajulishe DCI ama kituo cha karibu kilicho karibu, ama apige ama kutuma ujumbe mfupi kwa nambari 0772627435, 0203343412, 0202861097 ama atutumie baruapepe kwa [email protected],” DCI ikasema.