Habari za Kitaifa

Chebukati aombolezwa kama mtu mwenye msimamo, mwadilifu

Na ELVIS ONDIEKI February 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 1

RAIS William Ruto aliwaongoza Wakenya katika kumwombolewa aliyekuwa mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati, aliyekufa Alhamisi usiku, Februari 19, 2025 akimtaja kama “kiongozi mtiifu na aliyelihudumia taifa hili kwa uadilifu.”

“Nchi yetu imepoteza pakubwa kufuatia kifo chake,” akaongeza Dkt Ruto.

Katika ujumbe wake, Rais mstaafu Uhuru Kenyatta alisema hivi: “Kwa muda wote aliohudumu kama mwenyekiti wa IEBC alichangia pakubwa kuleta mageuzi bora katika masuala ya uchaguzi huku akikabiliana na changamoto ibuka kwa bidii.”

Naye Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula alimtaja Bw Chebukati kama “mwanasheria mashuhuri, mtetezi wa utawala wa sheria na mtumishi wa umma aliyejitolea kazini.”

Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen alisema Bw Chebukati atakumbukwa kwa “uongozi wake wenye msimamo, ujasiri na utiifu kwa Katiba.”

Kwa upande wake, Waziri wa Mazingira Aden Duale alisema maisha ya Chebukati yaliongozwa na “ujasiri, msimamo, uzingativu wa sheria, bidii na kujitolea kufanikisha kupatikana kwa demokrasia.”

Gavana wa Machakos Bi Wavinya Ndeti pia alimtaja Bw Chebukati kama “mtu mwenye maadili, bidii, kujitolea kuzingatia misingi ya kidemokrasia.”

Dkt Roselyn Akombe, ambaye aliwahi kuhudumu kama Kamishna wa IEBC chini ya Bw Chebukati aliweka ujumbe mfupi kwenye akaunti yake ya mtandao wa X akisema: “Pumzika Pema, Bw Mwenyekiti.”

Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini Kenya Bi Henriette Geiger alituma ujumbe wa pole, akiifariji taifa.

Inasadifu kwamba kifo cha Bw Chebukati kilitangazwa wakati ambapo kundi la waangalizi wa uchaguzi wa EU walikuwa wakijiandaa kuwatuhubia wanahabari kutangaza matokeo yao.

Imetafsiriwa na Charles Wasonga