NIPE USHAURI: Mtoto wa kupanga ametimu miaka 20 na anataka kumjua babake
Kwako shangazi. Nilipata mtoto kupitia kituo cha watoto mayatima kwa sababu sina uwezo wa kuzaa. Sasa ana miaka 20. Anaamini mimi ndiye mama yake na ameanza kuniuliza kuhusu baba yake. Nimwambie nini?
Ni haki ya mtoto huyo kujua asili yake. Itabidi umwambie ukweli na kumhakikishia kuwa umejitolea kumtunza kama mama yake mzazi. Ukimhadaa kisha baadaye ajue ukweli atakuchukia maisha yake yote.
Mke amekiri mtoto wa 2 si wangu, nifanye nini?
Kwako shangazi. Nina mke na watoto wawili. Nimekuwa nikishuku kuwa mtoto wa pili si wangu na hatimaye mke wangu ameungama baada ya kukana kwa muda mrefu. Anajuta sana na ameniomba msamaha. Nifanye nini?
Hilo ni kosa kubwa sana katika ndoa. Hata hivyo, mke wako ameungama kosa lake na anajuta. Shauri moyo wako uone iwapo unaweza kumsamehe badala ya kuvunja familia.
Nina miaka 19 lakini bado sina matiti na wenzangu wanayo
Kwako shangazi. Nina umri wa miaka 19. Wasichana wengi wa umri wangu wameota matiti lakini mimi bado, ni dalili tu. Nina wasiwasi, naomba ushauri wako.
Kwa umri wako huo, unafaa kuwa umeota matiti. Hata hivyo, watu wameumbwa kwa namna tofauti. Kama umeona dalili, ina maana kuwa hatimaye utakuwa sawa. Kuwa na subira na uondoe wasiwasi.
Nimegundua mpenzi wangu huwa na kimada kila wikendi
Mambo shangazi? Nimekuwa nikimshuku mpenzi wangu kwa sababu wikendi huwa hapatikani. Wikendi iliyopita nilimpigia simu ikapokewa na wanaume na akanionya nimkome mpenzi wake. Nifanye nini?
Sasa umejua ni kwa nini mpenzi wako huwa hapatikani wikendi. Aliyepokea simu ndiye mpenzi wake wa dhati, wewe ni mpango wa kando tu. Najua umeumia moyoni lakini huna budi ila kuachana naye.