Gharama ya maisha ingali kero kwa wengi – Ripoti
GHARAMA ya juu ya maisha ingali kikwazo kikuu kinachozuia Wakenya wengi kuwekeza katika biashara au kuweka akiba kwa manufaa ya siku zijazo, kulingana na ripoti ya hivi punde kuhusu hali ya kifedha ya raia nchini.
Ripoti iliyotolewa Ijumaa, Machi 14, 2025 kufuatia utafiti ulioendeshwa na kampuni ya kutoa mikopo kidijitali, Tala, inafichua kuwa asilimia 92 ya Wakenya wanasema kupanda kwa bei za bidhaa za kimsingi kunaathiri bajeti zao kiasi cha wao kutoweza kuweka akiba.
Kulingana na ripoti hiyo kwa jina “MoneyMarket 2025 Report”, hali hiyo ndiyo imechangia idadi kubwa ya Wakenya, wakiwemo walioajiriwa, hutegemea mikopo kukimu mahitaji yao ya kimsingi.
“Kwa hivyo Wakenya tisa kati ya 10 waliohojiwa ndani ya miezi sita iliyopita walisema wanakabiliwa na changamoto za kifedha. Asilimia 92 kati yao wamekimbilia mikopo ya kidijitali huku asilimia 35 wakikopa kutoka benki. Nao asilimia 21 hukopa kutoka kwa vyama vya akiba na mikopo na vyama vya ushirika, asilimia 21 wakikopa kutoka kwa serikali,” inaeleza ripoti hiyo.
Akiongea wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo katika mkahawa wa Serana Nairobi, Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Tala Annstella Mumbi alisema ipo haja ya Wakenya kupewa elimu kuhusu matumizi ya fedha.
“Ingawa gharama ya maisha ingali juu huku mapato yakipungua, huu ndio wakati mwafaka wa Wakenya kuwezeshwa katika masuala ya kifedha. Nasisitiza kuwa uwe umeajiriwa, uwe umejiajiri, ukiwa mfanyabiasha, mwanafunzi au yeyote anayehitaji kuwekeza, unahitaji uhamasisho au elimu kuhusu njia bora za usimamizi wa fedha,” akaeleza Bi Mumbi.
Kwa upande wake Menaja wa Idara ya Kulinda Masilahi ya Wateja katima Mamlaka ya Kusimamia Ushindani sawa wa Kibiashara Nchini (CAK) Boniface Kamiti alitoa changamoto kwa kampuni za utoaji mikopo kutoa mafunzo faafu kwa wateja wao.
“Wajibu wenu sio kutoa mikopo pekee, bali mnapaswa kusaidia wanaokopa kuelewa jinsi ya kutumia mikopo hiyo ipasavyo ili kujijengea mustakabali thabiti wa kifedha siku za usoni,” Bw Kamiti akaeleza.
Taswira inayotolewa na ripoti hii ni tofauti kabisa na ile ambayo serikali ya Kenya Kwanza imekuwa ikichora nyakati hizi kwamba gharama ya maisha imepungua.
Rais William Ruto, Naibu wake Kithure Kindiki na wakuu wengi wametaja kupungua kwa kiwango cha mfumko wa bei kutoka asilimia 9 mwaka 2022 hadi asilimia 3.5 Januari 2025, kushuka kwa bei ya mafuta na kuimarika kwa thamani ya shilingi ya Kenya dhidi ya sarafu za kigeni kama kiashirio cha kupungua kwa gharama ya maisha.