Joto lapanda Gor Dolphina, Rachier wakiwania uenyekiti
KAMPENI tayari zimeanza katika kambi ya Gor Mahia huku Mwenyekiti wa sasa Ambrose Rachier akitarajiwa kutifuana vikali na Mwekahazina wa klabu Dolphina Odhiambo katika uchaguzi wa klabu mnamo Aprili 13.
Jumatatu, Rachier alizindua mwongozo wa uchaguzi wa klabu na kusisitiza kuwa atagombea kiti chake tena. Rachier anayefahamika kama ADOR (Ambrose Dickens Otieno Rachier) alisema kuwa katiba ya klabu inamruhusu kuwania tena licha ya kuwa ameongoza klabu hiyo tangu 2009.
Alisema pia uamuzi wa Jopo la Kutatua Mizozo ya Michezo mnamo Januari 15, 2025 pia unamruhusu awanie ‘muhula wa pili”. Uchaguzi huo utatanguliwa na Mkutano wa kila mwaka, AGM na unatarajiwa utafanyika ukumbi wa Nyayo kuanzia saa moja asubuhi.
“Niko kwenye kinyángányo na nimesoma kifungu cha 20 kwenye katiba ya 2019. Tuliandaa uchaguzi wa kwanza mnamo 2020, tumehudumu muhula moja wa miaka minne kwa hivyo, tunaruhusiwa kuwania muhula wa pili,” akasema Rachier.
Kiongozi huyo alisema hamakinikii mahasidi na jambo muhimu kwake ni kuwa Gor inasakata soka ya kumezewa mate na kushinda mataji. Aliwataka wale ambao wanapinga uwanizi wake waelekee kortini.
KÓgalo imeshinda mataji 21 ya Ligi Kuu (KPL) na ni timu ya kwanza Kenya kushinda Kombe la Mashirikisho Afrika (CAF) mnamo 1987 baada ya kutinga fainali mnamo 1979.
Hata hivyo, Rachier ameanza kupata upinzani mkali kutoka kwa Dolphina Odhiambo ambaye hawajakuwa wakipatana naye kwenye uongozi wa klabu hiyo tangu wachaguliwe 2020.
Dolphina alisema kuwa yupo tayari kupambana na Rachier debeni akijitapa kuwa ndiye atakuwa mwokozi wa klabu kutoka kwa changamoto zinazoizonga.
Amepinga bodi ambayo ilitangazwa na Rachier kusimamia uchaguzi, akisema kuwa majina yaliyotangazwa ni wandani wa mwenyekiti huyo wa Gor.
“Huwezi kuwa refa na tena mwaniaji, naomba msajili wa michezo atupatie kamati ya kuandaa uchaguzi. Watu hawa wanastahili kupigwa msasa wakati wa mkutano wa kila mwaka ilhali mkutano huo tena utaandaliwa siku ya uchaguzi,” akasema kwenye mkutano na wanahabari jana.
“Niko tayari kumenyana naye kwa sababu najua changamoto ambazo zipo na sitazitoroka. Uongozi ni kuonyesha mwelekeo na mwongozo bora, nipo tayari sana na nina hakika nitapata ushindi,” akaongeza.
Iwapo atafaulu, atakuwa mwenyekiti wa kwanza wa Gor tangu klabu hiyo ianze mnamo 1968.