Waititu aomba dhamana kwa mara ya pili
ALIYEKUWA Gavana wa Kiambu, Ferdinand Waititu ‘Babayao’, ambaye kwa sasa yuko gerezani, amewasilisha ombi jipya la kutaka kuachiliwa kwa dhamana akisubiri uamuzi wa rufaa anayopinga hukumu na adhabu aliyopewa.
Hii ni mara ya pili kwa mwanasiasa huyo kujaribu kupata uhuru wake baada ya Jaji Lucy Njuguna kukataa ombi lake la kwanza mnamo Machi 3, 2025.
Akikataa kumuachilia Waititu kwa msingi wa afya, Jaji Njuguna alisema mfungwa huyo hakutoa msingi thabiti wa kisheria kuhalalisha kuachiliwa kwake kutoka gerezani.
Waititu, ambaye sasa amewaajiri mawakili Kibe Mungai na Ndegwa Njiru kushughulikia rufaa yake, anadai kwamba hakuhukumiwa kihalali kwa kuwa mashtaka ya ufisadi dhidi yake yalikuwa na dosari.
Awali, alikuwa akiwakilishwa na mawakili Danstan Omari, Shadrack Wambui, na Samson Nyaberi.
Waititu anasema rufaa yake ina nafasi kubwa ya kufanikiwa na kwamba hukumu ilikuwa na mbinu mbili, kwani alipewa chaguo la kulipa faini na akishindwa atumikie kifungo gerezani.
Katika ombi lake jipya, Waititu anasisitiza kwamba hawezi kutoroka na yuko tayari kufuata masharti yoyote ambayo mahakama itaweka ili kuhakikisha anaachiliwa huru “ikiwemo kutoa mdhamini anayeaminika na anayekubalika.”
Akiwasilisha ombi hilo, wakili Mungai alimwomba Jaji Njuguna kuthibitisha kwamba rufaa iliyowasilishwa Machi 11, 2025, ilipokelewa rasmi.
Mfungwa huyo anasema kuwa pesa alizopokea kutoka kwa kampuni ya Testimony Enterprises Limited (TEL) inayomilikiwa na Charles Chege Mbuthia zilikuwa Sh133,399,776.57.
Waititu analaumu upande wa mashtaka kwa kuwasilisha ushahidi kwamba alipokea Sh147 milioni.
“Kuna tofauti kubwa kati ya ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka kama ulivyoorodheshwa kwenye hati ya mashtaka na taarifa za benki, jambo ambalo linapunguza uzito wa ushahidi wa mashtaka na kuathiri uaminifu wake,” anasema Waititu katika ombi lake jipya la dhamana.
Zaidi ya hayo, Waititu anasema kuwa Kifungu cha 50 cha Katiba kinatambua kuwa hukumu inaweza kubatilishwa na mahakama ya juu, hivyo hakuna sababu ya mfungwa kuteseka akisubiri kusikilizwa kwa rufaa yake.