Habari za Kitaifa

Kioni: Matiang’i aliomba tiketi ya Jubilee kumenyana na Ruto 2027

Na BENSON MATHEKA March 26th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

ALIYEKUWA waziri wa usalama wa ndani Dkt Fred Matiang’i aliomba tiketi ya chama cha Jubilee kupeperusha bendera ya kura ya rais katika uchaguzi mkuu wa 2027, Katibu Mkuu wa chama hicho Jeremiah Kioni, amesema.

Akitetea uamuzi wa chama hicho kumuunga mkono Bw Matiang’i, kama mgombea wake wa urais katika uchaguzi wa mwaka 2027, Bw Kioni alisema kufikia sasa ni waziri huyo wa zamani pekee anayemezea mate tiketi ya chama hicho kugombea urais.

“Matiang’i ndiye kufikia sasa ameeleza azma ya kutumia tiketi ya chama cha Jubilee kugombea urais na ataongea kuhusu hili katika siku zijazo. Hatutangoja kwa muda mrefu, akihisi yuko tayari, atatangaza rasmi,” Kioni alieleza.

Hata hivyo alisema chama hakijafungia yeyote aliye na nia ya kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho kinachoongozwa na aliyekuwa rais uhuru Kenyatta. “Mtu yeyote anaweza kuwa na nia ya kuwania urais, na Matiang’i amefanya hivyo tu,” aliongeza.

Akizungumza Jumatatu jioni katika mahojiano na runinga ya TV47, Kioni chama kiliamua kumpa idhini moja kwa moja kwa kuwa mwanasiasa pekee aliyewasilisha azma yake kuwania urais kwa tiketi ya chama cha Jubilee.

Kioni pia alibainisha kuwa Matiang’i atatoa tangazo rasmi hivi karibuni kuhusu azma yake ya kuwania urais na kujibu maswali muhimu yanayohusiana na hatua yake hiyo.

Licha ya Matiang’i kuwania nafasi hiyo, Kioni alihakikishia Wakenya kuwa tiketi ya Jubilee bado iko wazi, na mtu yeyote aliye na azma kama hiyo anaweza kuwasiliana na uongozi wa chama.

“Ikiwa unataka kuwania, tuna wanachama milioni 7, na yeyote anayetaka kuonyesha nia bado ana nafasi. Kazi ya chama ni kumuuza mgombeaji,” alisema Kioni huku akifichua kuwa waziri huyo wa zamani ni mwanachama wa chama cha Jubilee.

“Ikiwa tutapata watu wengine wenye nia ya kugombea, tutawazingatia pia. Nimekuwa nikijaribu kuwashawishi wengine pia na kuwauliza kwa nini hawataki,” aliongeza.

Baadhi ya wazee kutoka Kaunti ya Kisii wameunga mkono azma Dkt Matiang’i kuwania urais katika uchaguzi mkuu ujao.

Wazee hao, pia walidokeza kuwa Dkt Matiang’i atarejea humu nchini hivi karibuni kubuni mikakati zaidi ya kufanikisha azma yake inayolenga kumng’atua mamlakani Rais William Ruto

Wakiongozwa na aliyekuwa spika wa bunge la kaunti ya Kisii, Bw David Kombo, wazee hao wanaotoka ukoo wa Dkt Matiang’i walitaja mfano wa utendakazi mzuri wa waziri huyo alipokuwa akihudumu katika serikali ya rais mstaafu Uhuru Kenyatta kama dhihirisho anatosha kuwa rais.

Walisema ufanisi ulioafikia Dkt Matiang’i katika wizara za Habari, Mawasiliano na Teknolojia (ICT), Elimu na Masuala ya Ndani ni sababu tosha za kiongozi huyo kupewa jukumu la kuliongoza taifa.

“Tuna imani Kenya haihitaji tu kiongozi mwenye maono bali pia mwenye ujuzi, mwadilifu na asiye fisadi. Dkt Matiang’i anazo sifa hizi. Kujitolea kwake katika utoaji wa huduma kwa raia na azma yake ya kuona Kenya yenye ufanisi, thabiti na yenye umoja si kitu cha kupingwa,” Bw Kombo alisema.