Seneta Tabitha ataka Kihika ampokeze naibu wake mamlaka
SENETA wa Nakuru Tabitha Karanja amejitosa katika mzozo kuhusu kutokuwepo kwa Gavana Susan Kihika akiwataka madiwani kuingilia kati ili kuzuia kutokea kwa mgogoro mkubwa katika kaunti hiyo.
Akiongea na wanahabari mjini Naivasha, Bi Karanja alitofautiana na kundi moja la wabunge wanawake waliomtetea Kihika akisema kutokuwepo kwake kumesababisha ombwe la uongozi, kukwamisha utekelezaji wa miradi na kutoa mwanya wa usimamizi mbaya wa fedha za umma.
Seneta Karanja alieleza kuwa kutokana na kutokuwepo kwa gavana huyo hospitali kadhaa zinakumbwa na uhaba wa dawa na vifaa vya matibabu huku wakandarasi wakikosa kulipwa.
Aliungama kuwa Gavana Kihika alijifungua watoto pacha lakini akasisitiza kutokuwepo kwake kwa muda wa mwaka mmoja ni kinyume cha sheria inayotoa likizo ya miezi mitatu ya kujifungua.
“Tunampongeza Gavana kwa kupata watoto pacha. Hiyo ni baraka. Lakini kutokuwepo kwake kwa muda mrefu kunasababisha mzozo. Anafaa kumkabidhi rasmi mamlaka naibu wake ili apate muda wa kutosha kupata afueni,” Bi Karanja akasema, huku akiandamana na viongozi kadhaa wa Kaunti ya Nakuru.
Kauli ya seneta huyo imejiri baada ya Naibu Gavana David Kones na kundi la wabunge wanawake kumtetea Gavana Kihika wakisema anahitaji muda kupata afueni ya kutosha baada ya kujifungua.
Lakini Karanja na wakosoaji wengine wa kiongozi huyo wakiwemo wakazi Esther Njoko na Naomi Njoki, walipuuzilia mbali utetezi huo, wakitaja kudorora kwa shughuli za utoaji huduma katika kaunti hiyo.
Seneta huyo aliwataka madiwani kutekeleza wajibu wao kikatiba wa kuhakikisha kuwa kaunti hiyo inaendeshwa inavyopasa kwa manufaa ya wananchi.
Bi Esther Njoko alihoji uamuzi wa Kihika wa kujifungua nchini Amerika, akisema hiyo inaonyesha kuwa hata yeye hana imani na huduma zinazotolewa katika hospitali za Kaunti ya Nakuru.