Ruto azungumza na Kiir na Museveni kuhusu Sudan Kusini baada ya Machar kukamatwa
RAIS William Ruto, Alhamisi, Machi 27, alizungumza kwa njia ya simu na Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir, muda mfupi baada ya kukamatwa kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa nchi hiyo, Riek Machar.
Kulingana na Rais wa Kenya, mazungumzo hayo yalihusu mazingira yaliyopelekea kukamatwa kwa Machar, ambaye amekuwa mpinzani wa muda mrefu wa Kiir kisiasa.
Katika taarifa fupi, Rais Ruto alieleza kuwa pia alizungumza kwa nyakati tofauti na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, kuhusu suala hilo tata la kukamatwa kwa Machar.
Baada ya mashauriano hayo, Rais Ruto alifichua kuwa ameamua kutuma mjumbe maalum kwenda Sudan Kusini kwa mazungumzo, ili kusaidia kutuliza hali.
“Nilifanya mazungumzo ya simu na Rais Salva Kiir kuhusu hali iliyopelekea kukamatwa na kuwekwa kizuizini kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Sudan Kusini, Riek Machar,” Ruto alieleza.
“Baada ya mashauriano na Rais Museveni na Waziri Mkuu Abiy, nimeamua kumtuma mjumbe maalum Sudan Kusini kwa mazungumzo ili kupunguza mivutano na kutupa taarifa ya hali ilivyo,” aliongeza.
Machar alikamatwa Jumatano, Machi 26, na kikosi cha maafisa wa usalama waliokuwa na silaha, ambao walivamia makazi yake jijini Juba, mji mkuu wa Sudan Kusini. Walimzuia na kuwanyang’anya walinzi wake silaha kabla ya kumweka kizuizini.
Baada ya kukamatwa, Machar aliwekwa chini ya ulinzi wa polisi pamoja na mkewe, Angela Teny, ambaye pia ni Waziri wa Masuala ya Ndani na Uratibu wa Serikali ya Sudan Kusini.
Kukamatwa kwake kulithibitishwa na Reath Muoch Tang, mshirika wa Machar, ambaye alilaani hatua hiyo akidai kuwa ni kinyume cha Katiba na kwamba kibali cha kukamatwa kwake hakikutoa mashtaka yaliyo wazi.
Saa machache baada ya Machar kukamatwa, Serikali ya Amerika ilitoa taarifa ikitaka aachiliwe mara moja ili kuzuia hali kuzorota zaidi katika nchi hiyo iliyokumbwa na migogoro kwa muda mrefu.
“Tuna wasiwasi kutokana na ripoti kwamba Makamu wa Kwanza wa Rais wa Sudan Kusini, Machar, amekamatwa. Tunamsihi Rais Kiir kubatilisha hatua hii na kuzuia kuendelea kwa mzozo huu,” ilisema sehemu ya taarifa ya Wizara ya Masuala ya Nje ya Amerika inayohusika na Afrika.