Chanzo cha mvutano wa Raila na Orengo
HATUA ya Gavana wa Siaya James Orengo kukaidi kiongozi wa ODM Raila Odinga kwa kuungana na Rais Ruto chini ya Serikali Jumuishi zimepokewa kwa hisia tofauti huku wadadisi wa siasa wakisema zimedhihirisha waziri mkuu huyo wa zamani havumilii wanaomuasi.
Uhusiano kati ya Raila na Orengo ni wa muda mrefu, wa kuvutia, na mara nyingine wenye mivutano ya kisera na misimamo. Tofauti zao zilianza miaka ya 1990 katika chama cha Ford Kenya, wakati wa mapambano ya uongozi wa chama hicho baada ya kifo cha Jaramogi Oginga Odinga.
Orengo alikuwa na mtazamo wa kisera wa kuimarisha demokrasia ya ndani ya chama, huku Raila akionekana kutumia ushawishi wa kisiasa na umaarufu kujijenga kama mrithi wa kisiasa wa baba yake.
Hatua hiyo ilimfanya Orengo kujitenga na kujiunga na Social Democratic Party (SDP) mwaka 2002, ambapo aliwania urais.
Raila wakati huo alikuwa amejiunga na muungano wa Narc.Katika mazungumzo ya upatanishi kufuatia uchaguzi mkuu wa 2007, Orengo alikuwa mmoja wa washauri wakuu wa kisheria wa Bw Odinga na akateuliwa waziri wa ardhi katika serikali ya mseto ambayo Raila alikuwa waziri mkuu.
Wawili hao walionekana kudumisha uhusiano mzuri hadi 2018 Raila alipofanya handisheki na Uhuru Kenya na kuanzisha Mpango wa Maridhiano (BBI) ambao Orengo hakuchangamkia.
“Orengo kwa mara nyingine alionyesha tofauti ya kimtazamo. Ingawa hakupinga BBI moja kwa moja, alionekana kuwa mwangalifu sana kuhusu vipengele vya sheria na utaratibu wa kikatiba uliotumiwa,” asema mchanganuzi wa siasa Dkt Isaac Gichuki.
Akiwa Seneta wa Siaya wakati huo, Orengo aliwahi kusema hadharani kuwa ‘sheria ni msumeno; hukata pande zote.’ Alikuwa miongoni mwa viongozi wa ODM waliotaka BBI izingatie Katiba, hata kama ilikuwa ni mradi wa Raila na Uhuru.
Ingawa wafuasi wengi wa ODM waliona kauli hiyo kama usaliti, ukweli ni kwamba Orengo alikuwa akisisitiza tu umuhimu wa kuzingatia misingi ya sheria na hatimaye BBI ilizimwa na Mahakama kwa kuwa kinyume cha Katiba.
Kwa sasa, tofauti zake na Raila zimeibuka kwa nguvu zaidi kufuatia kuundwa kwa Serikali Jumuishi kati ya Ruto na Raila na duru zinasema huenda akanyimwa tiketi ya ODM katika uchaguzi mkuu wa 2027.
Orengo amekuwa akikosoa vikali Serikali Jumuishi hata mbele ya Raila na Ruto. Akiwahutubia wakazi wa Siaya wakati wa mazishi ya aliyekuwa mlinzi wa Raila George Oduor, alisema: “Hatuwezi kuwa watu wa kusifu kila mara. Tukikosa kusema ukweli, hatutakuwa na taifa.”
Kauli hiyo imezua hasira kutoka kwa viongozi wa ODM hasa walio serikalini na familia ya Odinga.Waziri wa Kawi, Opiyo Wandayi na Oburu Oginga kaka ya Raila, wamemtaka Orengo kuwa mtiifu kwa uamuzi wa chama.
Lakini kwa Orengo, hali ni tofauti – anaona historia ikijirudia. Raila, kwa mtazamo wake, bado anatumia ushawishi wake kushinikiza mikataba ya kisiasa ambayo haihusishi mashauriano ya kina na viongozi wa chama.
“Ni dhahiri kuwa James Orengo anamjua Raila kwa undani kuliko wanaomkosoa baadhi ambao walizaliwa wawili hao wakiogelea katika mawimbi ya siasa,” asema Dkt Gichuki. Anasema tofauti kati ya Orengo na Raila si jambo jipya.
“Ni mwendelezo wa tofauti zao za kiitikadi na kimkakati ambazo zimekuwepo kwa zaidi ya miongo miwili. Wawili hao wanajuana vyema na wanaotumiwa kuingilia tofauti zao huenda wakaaibika,” asema.