Punguza vyakula hivi, vitakufanya ufe mapema
ULAJI wa vyakula vilivyosindikwa kupita kiasi unahusishwa moja kwa moja na ongezeko la hatari ya kufa mapema, utafiti mpya umebaini. Kulingana na utafiti huo wa kimataifa, kifo kimoja kati ya saba katika baadhi ya nchi kinaweza kuhusishwa moja kwa moja na matumizi ya vyakula hivi.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), vyakula vilivyosindikwa kupita kiasi ni vile vinavyotengenezwa hasa kutoka kwa viambato vya viwandani na viongeza ladha bandia na mafuta. Mifano ni pamoja na vinywaji vyenye sukari nyingi, vitafunwa vya viwandani, vyakula vilivyopakiwa tayari kwa matumizi, na nafaka za kifungua kinywa.
Licha ya kuwa rahisi kupatikana na kutumia, vyakula hivi vina kalori nyingi lakini lishe hafifu, na vimetengenezwa ili kuchochea kula kupita kiasi. “Kwa walaji wengi, hasa mijini, vyakula hivi vimekuwa sehemu ya kawaida ya lishe badala ya kuwa vichangamsho vya nadra,” utafiti unasema.
Watafiti walifanya uchambuzi wa kina wa takwimu kutoka nchi mbalimbali, zikiwemo zile za kipato cha juu kama Amerika na Uingereza, pamoja na zile za kipato cha kati kama Brazil na Colombia. Matokeo yalionyesha kwamba kwa kila ongezeko la asilimia 10 ya ulaji wa vyakula hivyo katika lishe ya mtu, hatari ya kufa mapema uongezeka kwa asilimia 3.
Nchini Amerika pekee, vifo 124,107 vya mapema kila mwaka vinaweza kuhusishwa na ulaji kupita kiasi wa vyakula vilivyosindikwa, huku Uingereza ikiwa na vifo 17,781 kwa mwaka. Nchini Colombia ambako matumizi ya vyakula hivi ni ya chini, ni asilimia 4 tu ya vifo vinavyohusishwa, huku Mexico na Chile zikiwa na asilimia 6.
Watafiti wanatahadharisha kuwa madhara ya vyakula hivi hayaishii kwenye virutubishi hatari tu kama chumvi, sukari na mafuta yasiyo na afya, bali pia kutokana na mabadiliko yanayofanyika wakati wa usindikaji viwandani. Viongeza kama rangi bandia, kusababisha ladha vina athari kubwa kwa afya.
Utafiti huo unatoa wito kwa serikali na mashirika ya afya duniani kuchukua hatua madhubuti. Hii ni pamoja na kuhimiza ulaji wa vyakula asilia na vilivyosindikwa kidogo, kuweka masharti ya kuwepo kwa alama za tahadhari mbele ya pakiti ya bidhaa pamoja na kuweka kodi kwa bidhaa zisizo na afya.
Gideon Ogutu, mtaalamu wa lishe katika Taasisi ya Kimataifa ya Masuala ya Kisheria, anasema kuwa kuweka alama za tahadhari mbele kutawasaidia walaji kufanya maamuzi sahihi. Hata hivyo, anasema Kenya bado haijatekeleza utaratibu huu, huku mashauriano ya sheria husika yakiwa bado katika hatua za awali. Kuna mvutano kuhusu kama alama hizo zinafaa kuwa za hiari au lazima, huku wazalishaji wa vyakula hivyo wakiweka upinzani mkubwa.
Kwa mujibu wa WHO, magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari, shinikizo la damu na saratani yamekuwa chanzo kikuu cha vifo na kulazwa hospitalini Kenya. Kwa sasa, mzigo huu unaendelea kuongezeka kutokana na ulaji wa vyakula visivyo na afya pamoja na mtindo wa maisha usio na mazoezi.
Utafiti huu ni ishara tosha kwamba hatua za haraka zinahitajika ili kulinda afya ya umma dhidi ya athari mbaya za vyakula vilivyosindikwa kupita kiasi.