Habari za Kitaifa

Maeneo haya yatakumbwa na upepo mkali kwa siku tatu

Na BENSON MATHEKA May 23rd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

IDARA ya Utabiri wa Hali ya Hewa  Kenya imeonya Wakenya wanaoishi katika Pwani, maeneo ya chini ya kusini-mashariki, na maeneo ya kaskazini-magharibi ya nchi kujiandaa kwa upepo mkali katika kipindi cha siku tatu zijazo.

Mnamo Ijumaa, Mei 23,  Idara hiyo  ilionya wakazi wa Marsabit, Turkana, Samburu, Isiolo, Mandera, Wajir, Garissa, Kitui, Makueni, Taita Taveta, Tana River, Lamu, Kilifi, Mombasa, na Kwale kuwa waangalifu dhidi ya upepo mkali ambao unaweza kusababisha uharibifu.

Kulingana na idara hiyo, upepo mkali kutoka kusini unaozidi kasi ya knot 30 (mita 15.4 kwa sekunde) ulitarajiwa kuvuma katika Pwani, maeneo ya chini ya kusini-mashariki, na kaskazini-magharibi mwa Kenya kuanzia Ijumaa, Mei 23, 2025.

Kasi ya upepo huo inatarajiwa kuongezeka hadi zaidi ya knot 35 (mita 18.0 kwa sekunde) Jumamosi, Mei 24, na Jumapili, Mei 25, kabla ya kupungua hadi knot 25 (mita 12.9 kwa sekunde) Jumatatu, Mei 26.

Vilevile, idara hiyo iliwaonya Wakenya wanaoishi katika kaunti za Pwani za Tana River, Mombasa, Kwale na Kilifi kujiandaa kwa mawimbi makubwa ya baharini kwa siku tatu zijazo.

Katika onyo hilo,  idara ilieleza kuwa mawimbi ya bahari yanatarajiwa kufikia urefu wa zaidi ya mita 2 katika maji ya Pwani kuanzia Ijumaa, Mei 23 hadi Jumapili, Mei 25, kabla ya kushuka hadi chini ya mita 2 siku ya Jumatatu.

“Wakazi wa maeneo yote yaliyotajwa, wanashauriwa kuwa waangalifu dhidi ya uwezekano wa upepo mkali sana na mawimbi katika Bahari ya Hindi,”  Idara ilionya na kuongeza:”Upepo mkali unaweza kung’oa paa na kuharibu majengo. Mawimbi makubwa yanaweza kupunguza uwezo wa kuona na kuathiri shughuli za baharini.”

Kuhusu uhakika wa kutokea kwa hali hiyo, idara ilieleza kuwa kuna uwezekano wa wastani, kwa asilimia kati ya 33 hadi 66.

Onyo hilo linajiri wakati maeneo kadhaa nchini bado yanakumbwa na mvua kubwa inayosababisha mafuriko na kufanya maelfu ya familia kuhama makazi yao.

Katika utabiri wa hali ya hewa wa hivi karibuni, Idara ilieleza kuwa mvua itaendelea kunyesha katika maeneo ya Nyanda za Juu Mashariki na Magharibi mwa Bonde la Ufa, Bonde la Ziwa Victoria, Bonde la Ufa, Pwani na kaskazini-magharibi mwa Kenya.