• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:53 PM
Maafisa wa NTSA wanaoshukiwa kuhusika kwa mauaji ya DusitD2 waachiliwa

Maafisa wa NTSA wanaoshukiwa kuhusika kwa mauaji ya DusitD2 waachiliwa

Na RICHARD MUNGUTI

MAAFISA watano wa Mamlaka ya Kitaifa ya Usalama wa Uchukuzi (NTSA) waliotiwa nguvuni na kuzuiliwa kuhusishwa na shambulizi la hoteli ya DusitD2 ambapo watu 21 waliuawa waliachiliwa Ijumaa.

Hakimu mkazi Bi Muthoni Nzibe alifahamishwa na upande wa mashtaka kwamba hakuna ushahidi uliopatikana kuwahusisha moja kwa moja maafisa hao wa NTSA na shambulizi hilo lililotekelezwa na magaidi wa Al Shabaab mtaani Westlands, Nairobi.

Bi Nzibe alikuwa ameamuru watumishi hao sita wa wazuiliwe kwa muda wa siku 30 kuwasaidia polisi kukamilisha uchunguzi.

“Naomba hii mahakama iwaachilie washukiwa kwa vile hakuna ushahidi wa kuwahusisha na shambulizi hilo,” kiongozi wa mashtaka alimweleza Bi Nzibe Ijumaa alasiri.

Hakimu aliombwa awaachilie washukiwa hao watano kisha awaamuru wawe wakipiga ripoti kwa afisi ya kupambana na ugaidi ATPU kila Alhamisi hadi maagizo mengine yatolewe.

Hakimu alifahamishwa wafanyakazi hao wa NTSA walishukiwa waliwasaidia magaidi hao kwa kuandikisha magari mawili tofauti wakitumia nambari moja ya usajili – KCN 240E.

Gari hili muundo wa Toyota Ractis, ndilo lilitumiwa na magaidi hao kwenda DusitD2 mnamo Januari 15, 2019.

Watano kati ya maafisa hao sita wanadaiwa kuhusika kwenye kashfa ya kutengeneza nambari feki za usajili wa magari.

Bi Nzibe alielezwa na kiongozi wa mashtaka Bw Duncan Ondimu kuwa maafisa hao wa NTSA waliwasaidia magaidi hao kwa kuwapa nambari feki ya usajili.

“Naomba hii mahakama iwaruhusu polisi wawahoji washukiwa hawa kwa siku 30 ndipo ukweli ujulikane kuhusu kashfa ya utoaji nambari feki za usajili wa magari,” Bw Ondimu alimweleza hakimu washukiwa walipofikishwa mahakamani wiki iliyopita.

Wakili Dunstan Omari aliyewatetea maafisa hao wa NTS. Picha/ Richard Munguti

Lakini ombi hilo lilipingwa vikali na mawakili Dunstan Omari na Jotham Arwa waliosema muda unaoombwa na polisi ni mwingi na uchunguzi unaotakiwa kufanywa sio mwingi vile.

“Kuwapa polisi muda huo wa siku 30 ni ukandamizaji wa haki za washukiwa,” alisema Bw Omari.

Bw Arwa alimweleza hakimu kuwa mkurugenzi wa mashtaka ya umma anatakiwa kuwafikisha kortini washukiwa baada ya kukamilisha uchunguzi.

Bi Nzibe alikubalia ombi la DPP akisema polisi wanahitaji muda kukamilisha zoezi hilo.

Waliozuiliwa ni Bw Anthony Kadu, anayefanya kazi katika idara ya usajili. Kazi yake ni kuandikisha magari kwa wanunuzi wapya. Bi Jacqueline Githinji, mkurugenzi wa usajili na utoaji leseni, Bw Cosmas Ngeso, ambaye ni naibu wa Bi Githinji.

Wengine ni Bw Irving Irungu, Bw Stephen Kariuki, karani anayehusika na upeanaji wa nambari za usajili na Bw Charles Ndung’u anayefanya kazi katika idara ya utoaji wa hatimiliki za magari.

Wa mwisho ni Bw Augustine Mulwa Musembi aliyefikishwa kortini Jumatano. Polisi walikubaliwa kumzuilia Bw Musembi kwa muda wa mwezi mmoja.

Uchunguzi wa polisi ulibaini nambari ya usajili ya gari hilo -Toyota Ractis nambari ya usajili KCN 240E –  lililotumiwa na magaidi watano waliouawa limesajiliwa na gari lingine muundo tofauti lililopatikana Kitengela, Kaunti ya Kajiado.

Polisi wanasema usajili wa gari moja ni feki ama ulifanywa kwa njia ya udanganyifu.

Bw Musembi anahofiwa ndiye alisaidia katika usajili huo feki ilhali Bw Kadu anadaiwa ndiye alimwamuru Musembi kuandikisha tena nambari hiyo iliyotumiwa na magaidi hao.

Polisi waliomba muda kuwahoji maafisa hao wa NTSA na kuendeleza uchunguzi mwingine wa kina.

“Ni muhimu polisi kupewa muda kukamilisha uchunguzi na kubaini utengenezaji na utoaji wa nambari ya usajili inayopewa magari mawili tofauti,” korti iliombwa.

Hakimu aliamuru kesi hiyo itajwe Februari 28, 2019.

You can share this post!

Wauzaji wa nepi feki waachiliwa kwa dhamana

Mama ndani miaka 9 kwa kunajisi watoto wake kumfurahisha...

adminleo